Ulinzi mkali umeimarishwa katika Shule ya Melvin Jones Academy ambayo ni mwenyeji wa Tamsha la Kitaifa la Drama awamu ya mwaka huu wa 2025.
Ni wanafunzi na maafisa pekee wanaohudumu katika tamasha hilo wanaruhusiwa kuingia. Kwa sasa polisi wameshika doria huku wanahabari na wakazi wakizuiwa kuingia. Hali hii imetokana na Mchezo wa Kuigiza kwa jina ‘’Echoes of War’’ wa Shule ya Upili ya Butere lililoandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha UDA Cleophas Malala na ambalo limeibua utata.
Japo serikali ilikuwa imelipiga marufuku mchezo huo, Mahakama Kuu mjini Nyamira ilitoa uamuzi ulioruhusu uwe miongoni mwa michezo itakayoigizwa katika tamasha hizo za kitaifa.
Alhamisi jioni, kulikuwa na makabiliano baina na polisi na Malala baada ya maafisa wa polisi kumzuia kuingia katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kirobon iliyoko Kaunti ya Nakuru, walikokuwa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Butere wakisubiri kushiriki katika tamasha hilo linalofanyika Alhamisi.
Malala anayesemakana kukamatwa Jumatano wakati mvutano huo na polisi anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Eldama Ravine, katika Kaunti ya Baringo. Seneta huyo wa zamani anatarajiwa kufikishwa mahakamani baadaye Alhamisi ila mashtaka kamili dhidi yake hayajathibitishwa.