Wizara ya Afya imetangaza kuwasili kwa dozi 10, 700 za chanjo ya Mpox aina ya MVA-BN. Chanjo hizi zimewasili kufuatia ushirikiano baina ya Serikali ya Kenya, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Maambukizi ya Magonjwa CDC, Shirika la Afya Duniani WHO, Shirika la Kimataifa Linalowashughulikia Watoto, UNICEF na Muungano wa Kushughulikia Masuala ya Chango GAVI.
Waziri wa Afya Adan Duale amesema kuwasili kwa Chanjo hizo kutasaidia pakubwa katika kukabili maambukizi ya Mpox, ikizingatiwa chanjo ni njia mojapowa muhimu ya kukabili magonjwa yanayosambaa kwa haraka.
Duale amesema chanjo hiyo ni nyongeza tu katika mikakati iliyowekwa na serikali katika kukabili ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na ukaguzi katika maeneo 26 ya mipakani, kuwafuatilia watu wanaingia nchini kutoka mataifa mengine, kuwapima na kuwapa matibabu panapohitajika.
Waziri huyo amesema sasa serikali itapiga hatua kwani maambukizi ya Mpox yalikuwa yameongezeka kwa asilimia 100 tangu kisa cha kwanza kuripotiwa Desemba tarehe 31, mwaka 2024.
Tangu wakati huo visa 67 vya Mpox vimethibitishwa katika kaunti 13 nchini. Kaunti hizo ni Busia (22), Mombasa (12), Nakuru (10), Makueni (6), Bungoma (3), Nairobi (3), Kajiado (2), Taita Taveta (2), Kericho (2), Kilifi (2), Kiambu (1), Uasin Gishu (1) na Migori (1).
Miongoni mwa visa hivyo, wagonjwa arubaini na tisa (49) wamepona , kumi (10) wanaendelea kulazwa na saba (7) wanaendeela kuhudumia nyumbani. Ni mtu mmoja tu amethibitishwa kuaga dunia kutokana na Mpox. Chanjo ya MVA-BN imethibitishwa kuwa salama na kuzuia maambukizi. Ufanisi wa chanjo unakadiriwa kuwa asilimia 82 kwa dozi mbili zinazotolewa kwa muda wa wiki nne kati ya kila dozi.
Wizara imesema chanjo hiyo haitatolewa kwa kila mtu bali watakaofanywa kipaumble ni walio katika hatari. Kama vile; waliotangamana na wanaougua Mpox, walioyatembelea maeneo ambapo visa vya ugonjwa huo vimeripotiwa, pamoja na maafisa wa afya.
Ili kuzuia maambukizi zaidi wananchi wameshauriwa kuchukua tahadhari.