Maafisa 10 wa Serikali ya Kaunti ya Turkana wanaendelea kuzuiliwa baada ya kukamatwa Alhamisi kufuatia sakata ya wizi wa shilingi milioni 600.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud, fedha hizo ziliibwa kutoka kwa sehemu ya zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023 na 2023/2024.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Waziri wa Fedha wa Kaunti, Michael Eregae Ekidor, mwenzake wa Maendeleo ya Mji Peter Lomurukai, Mark Achila Ekiru, wa Barabara , Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi Samson Nakito na Mhasibu Mkuu Lillian Alaper Ateyo.
Wengine ni Annah Narot Longoli na Mumewe John Tioko Ekal, Abenyo Amathwel Etiir, Stephen Lowoton William Erex Aminit na Nangiro Edung Ichor.
EACC imesema washukiwa walikamatwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kina kuhusu wizi wa mali ya umma.
Abdi alisema, “The suspects are alleged to have abused their positions of trust and authority to embezzle public funds through collusion, procurement fraud, bribery and payment for fictitious contracts,”
Maafisa kadhaa wa kaunti wamelaumiwa kwa kutumia nyadhfa zao kufanya biashara na kaunti suala ambalo ni kinyume na sharia.
Tume hiyo ya EACC inasema Eregae ambaye ni mshukiwa mkuu amejipatia mali ya mamilioni ya pesa kwa njia isiyoeleweka tangu kuchaguliwa katika wadhfa huo. Wakati wa operesheni hiyo maafisa wa EACC walipata shilingi milioni 6.5 ndani ya gari la Eregae.
Washukiwa walirekodi taarifa katika ofisi za EACC mjini Lodwar.
Ikumbukwe tume hiyo ilipata agizo la mahakama Machi mwaka huu wa 2025 kuzifunga akaunti za Abenyo Amathwel Etiir, ambaye alikuwa mlinzi katika kaunti na anayehusishwa na kampuni zilizokuwa zikifanya kazi na kaunti kinyume na sharia.
Abdi alisema baada ya uchunguzi kukamilika, itabainika hatua zitakazochukuliwa dhidi ya washukiwa, kukiwamo kurejesha fedha zilizoibwa au kutwaa mali yao.