Ruth Kamande mwanamke aliyelishangaza taifa kwa kumuua mpenzi wake kwa kumdunga kisu mara ishirini na tano, mwaka 2015 atasalia gerezani.

Hii ni baada ya Mahakama ya Upeo kutupilia mbali ombi alilokuwa ameliwasilisha akitaka wanawake wanaotekeleza kosa au uhalifu wowote kutokana na kunyanyaswa au kuteswa na wapenzi wao kwa muda (Battered woman Syndrome) kutopewa hukumu sawa na wahalifu wengine.

Kamande aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja wakati wa mauaji hayo, alimdunga na kumuua Farid Halim Mohhamed aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na mitano mtaani Buruburu.

Mahakama ya Upeo imeamua kwamba “Battered woman syndrome” haijatambuliwa  kuwa utetezi wa pekee kisheria. Imesema inapaswa kutumika kusaidia au kuendeleza mojawapo ya zile zilizopo kama vile kujilinda (self-defense), uchokozi (provocation) au wazimu wa muda (temporary insanity). Hivyo, mahakama haina mamlaka ya kuipa hali hii hadhi ya kuwa utetezi pekee wa kisheria, kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kuingilia mamlaka ya kutunga sheria, ambayo kwa mujibu wa Katiba, ni ya Bunge.

Aidha Mahakama imesema iwapo upande wowote unataka kutumia “battered woman syndrome” wakati wa kesi, basi lazima ufahamishe mahakama mapema.

Katika uamuzi uliotolewa na majaji, Martha Koome, Philomena Mwilu, Isaac Lenaola, Smokin Wanjala, Mohammed Ibrahim, William Ouko na Njoki Ndungu ni kwamba iwapo utetezi wa kujilinda (self-defense) kunahusishwa na hali ya “battered woman syndrome”, basi viwango vya uthibitisho lazima vizingatie kanuni za kisheria zinazotumika katika aina hiyo ya utetezi

Kadhalika, mahakama ilieleza kuwa hoja ya “battered woman syndrome” ilitolewa kwa mara ya kwanza wakati wa kuidhinisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa, na haikuwahi kuwasilishwa wala kujadiliwa kwenye mahakama za awali.

Kufuatia uamuzi huu, Kamande atasalia gerezani anakohudumu kifungo cha maisha.