Mvutano unatokota baina ya Bodi ya Udhibiti wa Huduma za Maji (WASREB) na Serikali ya Kaunti ya Murang’a kufuatia hatua Kaunti kuchapisha notiSi katika gazeti moja nchini kufahamisha umma kuhusu mabadiliko ya ada za Huduma za maji.
Katika taarifa yake WASREB imesema tangazo hilo linakiuka Kifungu cha 72(1)(b) cha Sheria ya Maji ya mwaka 2016, ambacho kinaipa WASREB mamlaka ya kuchunguza, kupendekeza na kuidhinisha viwango vya ada za maji na majitaka kwa wanaotoa huduma katika kaunti.
Japo utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira ni jukumu lililogatuliwa, Katiba na Sheria ya Maji ya mwaka 2016 ndizo zinazoelekeza kuhusu umiliki, usimamizi na udhibiti wa huduma hizo.
Kifungu cha 70 cha Sheria ya Maji kinaiweka WASREB kama mdhibiti wa kitaifa, mwenye jukumu kuu la kulinda maslahi na haki za watumiaji.
Sehemu ya taarifa hiyo inasema, ‘’Section 158 of the Water Act 2016 provides that a County Government to give effect to the national water services standards and conditions set by the Regulatory Board for purposes of ensuring consumer protection and take into consideration the requirement relating to Tariffs gazetted by the Regulatory Board’’
Kifungu cha 158 kinazitaka serikali za kaunti kufuata viwango vya kitaifa vya huduma za maji na masharti yanayotolewa na WASREB, hasa kuhusu viwango vya ada.
Sasa, WASREB inasisitiza kuwa ndiyo pekee iliyo na mamlaka ya kuidhinisha na kuchapisha viwango vya ada ya huduma za maji. Wananchi sasa wameshauriwa kupuuza tangazo hilo, na kutambua kuwa mabadiliko yoyote halali ya viwango vya ada yatatangazwa na kuchapishwa rasmi na WASREB.