Uchunguzi wa kijeshi umebainisha kuwa ajali ya helikopta iliyomuua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Francis Ogolla na maafisa wengine, ilisababishwa na hitilafu ya injini.
Katika ripoti iliyotolewa Ijumaa na Wizara ya Ulinzi, helikopta aina ya Huey KAF 1501 ilitajwa kuwa na historia nzuri ya ufanisi , ikiwa imehusika katika misheni mbalimbali za kijeshi na mafunzo, zikiwamo safari za viongozi wa juu.
“Safari hiyo pia ilikuwa inaendeshwa na marubani waliobobea na waliohitimu. Hata hivyo, kwa mujibu wa walionusurika, marubani walijaribu kuitua helikopta hiyo kwenye eneo salama, lakini walishindwa kuidhibiti,” ripoti ilisoma.
Uchunguzi ulionesha kuwa kulikuwa na Engine Compressor Stall (Surge), hali inayolingana na ripoti za mashahidi waliokisikia kishindo kikubwa kutoka eneo la injini na kifaa cha kupima joto (MGT) kuonesha ongezeko la joto hadi nyuzi joto 914 °C.

Baada ya hapo, helikopta ilianza kuzunguka upande wa kushoto, na milio ya tahadhari ilisikika kabla ya kugonga ardhini.
Ripoti ilieleza kwamba, “Kwa kuzingatia ushahidi uliokusanywa, Bodi ya Uchunguzi imebaini kuwa ajali ya helikopta aina ya Bell UH-1H-II (Huey) KAF 1501 ilisababishwa na hitilafu ya injini.”
Jenerali Francis Ogolla alifariki Aprili 18, mwaka 2024, baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Kaben, Marakwet Mashariki. Helikopta hiyo ilikuwa imewabeba watu 12, wakiwamo maafisa wa ngazi ya juu. Mtu mmoja pekee ndiye aliyenusurika.
Ogolla aliteuliwa kuwa CDF kuchukua nafasi ya Jenerali Robert Kibochi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Mkuu wa Majeshi. Alisomea katika École Militaire de Paris, Chuo cha Ulinzi cha Kitaifa (NDC), na vyuo vikuu vya Egerton na Nairobi, ambako alipata shahada za uzamili katika masuala ya siasa, uhusiano wa kimataifa na amani.
Aliwaacha mke Aileenn Ogolla, watoto wawili na mjukuu mmoja.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) ndiye afisa wa kijeshi mwenye cheo cha juu zaidi katika Jeshi la Kenya na mshauri mkuu wa kijeshi kwa Rais na Baraza la Usalama la Kitaifa.