Wakristu Jumapili wanajumuika makanisani kwa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi. Jumapili ya Matawi ni mojawapo ya siku muhimu katika kalenda ya Kikatoliki pia katika baadhi ya Madhehebu kama Anglikana, Orthodox na Lutheran.  Siku hii huwa kumbukumbu ya Yesu Kristo kuingia kwa kishindo mjini Yerusalemu, akiwa amepanda punda ishara ya unyenyekevu na amani.

Katika mahojiano na Katekista Joseph Muteti (Katekista ni mtu aliyefunzwa rasmi kufundisha Imani ya Kikiristu hasa Katoliki, kwa waumini, wanaojiandaa kupokea sakramenti kama vile ubatizo, kipaimara, na ndoa) alieleza kuwa tukio hili linaonesha jinsi watu wa Israeli, hasa Wayahudi, walivyompokea Yesu kwa shangwe, wakipeperusha matawi ya mitende na kumtandikia mavazi njiani, wakisema: “Hosana Hosana! Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana!”

Matawi haya ya mitende ndiyo asili ya jina la siku hii “Jumapili ya Matawi.”

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa wale wale waliompokea kwa shangwe, siku chache baadaye walikuwa katika umati uliopaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Katekista  Muteti anasema kuwa tukio hili linawafundisha Wakristu kuhusu hatari ya unafiki na kubadilika-badilika kwa moyo wa mwanadamu. Anasema ‘’ Ni mwito kwa Wakiristu kuwa waaminifu katika imani na katika uhusiano wao na Mungu, bila kuyumbishwa na hali au hisia za wakati.’’

Mbali na hilo, Jumapili ya Matawi pia huwafundisha Wakristu kuhusu unyenyekevu wa Yesu. Ingawa alikuwa Mfalme wa Wafalme, hakuingia Yerusalemu kwa farasi wa kifalme wala akiwa na jeshi, bali kwa punda. Hili ni funzo la kina kwamba ukuu wa kweli hupatikana katika unyenyekevu na huduma. Matukio haya yanawakumbusha wakiristu kuwa hawapaswi kutafuta ukubwa wa dunia bali kufuata mfano wa Yesu wa kujitoa kwa upendo kwa ajili ya wengine.

Kadhalika, Muteti anaeleza yapo mambo muhimu katika siku hii hasa kwa Wakatoliki ambayo ni;

Katika Misa, matawi hubarikiwa kisha waumini huandamana nayo kwa heshima kama ishara ya ushindi na utukufu wa Kristo.

Pia kunafanyika usomaji mrefu  wa Injili unaoelezea mateso ya Yesu yaani (Passion reading).

Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa tafakari ya kina kuhusu ya mateso, kifo, na ufufuko wa Kristo.

Jumapili hii ya Matawi huashiria mwanzo wa Juma Kuu; yaani wiki ya mwisho ya maisha ya Yesu Kristu Kabla ya kusulubiwa na kufufuka kwake.

Muteti anasema ‘’Ni mwaliko kwa kila Mkristo kuingia katika wiki hii kwa moyo wa toba, sala, na matendo ya huruma.’’