Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga imewashauri Wakenya kujitayarisha kwa mvua kubwa itakayonyesha katika maeneo mbalimbali nchini mwishoni mwa wiki hii.
Kupitia taarifa Idara hiyo imesema Jumamosi na Jumapili mvua kubwa itanyesha katika maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, ikiwamo Nairobi.
Maeneo mengine yatakayopata mvua hiyo ni sehemu za chini za Kusini-Mashariki, Pwani, Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Mvua kubwa zaidi inatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na Bonde la Ufa ni pamoja na: Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi.

Taarifa hii inatolewa wakati mvua inayoendelea kunyesha jijini Nairobi na maeneo mengine imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu kama barabara.
Mwezi wa Aprili unafahamika kuwa wa kilele cha msimu wa Mvua za Masika, ambapo maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua ya wastani hadi juu ya kiwango cha kawaida.
Kwa maeneo ya Kaskazini, kiwango cha mvua kinachotambuliwa kama mwanzo wa msimu ni milimita 10 kwa siku tatu mfululizo.
Kilele cha msimu wa mvua katika ukanda wa Pwani kinatarajiwa kufikia mwezi Mei.