Huzuni imetanda katika eneo la Tach Asis, Konoin, Kaunti ya Bomet, baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 35 kuwaua kwa kuwakatakata wanawe wawili wa miaka 2 na 7.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Bomet, Edward Imbwaga, mshukiwa aliyejitambulisha kama Geoffrey Kipkemoi anadaiwa kutumia kisu cha jikoni kutekeleza unyama huo.

Miili ya watoto hao ilipatikana ikiwa imetupwa jikoni baada ya tukio hilo. Kulingana na ripoti ya polisi, mkewe mshukiwa hakuwa nyumbani wakati wa tukio hilo. Aligundua kilichotokea baada ya kufuata madoa ya damu yaliyomwelekeza hadi jikoni, na hapo ndipo alipowaarifu maafisa wa usalama.

Polisi walifika katika eneo la tukio, na wakapata kisu kinachoshukiwa kutumika. Miili ya watoto hao ilisafirishwa hadi Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Kapkatet inakosubiri kufanyiwa uchunguzi.

Mshukiwa amekamatwa na anaendelea kuziliwa huku uchunguzi ukiendelea.