Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed sasa anasema mafanikio yake makubwa yalikuwa ni kumtimua mamlakani aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua. Mbunge huyo wa Suna Mashariki Junet Mohhamed amesifia hatua ya Bunge la Kitaifa kufanikisha kuondolewa mamlakani aliyekuwa Naibu wa Rais Righathi Gachagua.

Akizungumza wakati wa hafla ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Raila Odinga, George Oduor katika eneo la Ndori, Kaunti ya Siaya Junet amemtaja Gachagua kuwa mkabila aliyekuwa na nia ya kuligawanya taifa.

Amesema ‘’ One of my biggest achievement katika bunge ambayo nimefanya was to impeach your deputy (akimweleza rais) kwa sababu yeye ndiye alikuwa anaongoza hii mambo ya ubaguzi, anasema hawa hawana shareholding, hawa wahame Kenya waende Uganda. Sisi watu wa Migori alituweka Tanzania hata sio Kenya. Mimi wakati hiyo motion ilikuja nilikuwa natembea kwa nyumba za wabunge usiku hata sio mchana nawaambia wekeni sign hapa huyu mtu aende’’

Aidha amemshtumu Gachagua akimtaja kuwa mnafiki hasa kuhusu kauli za kuikosoa serikali.

‘’Huyo alikuwa mtu hatari kwa nchi yetu. Saa hizi nikimwona akilialia kila mahali kwa TV nasikia vizuri  sana, naweka chai kwa kikome nasema wewe endelea kulia sisi tulilia zamani’’ Amesema Junet

Junet amewapongeza Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuamua kushirikiana akisema hatua hiyo imepunguza joto la kisiasa nchini.

‘’Your excellency kitu moja umefanya pamoja na Baba ni kusaidia kuleta Wakenya pamoja. Sisi saa hii tuko na Chairman ya Budget kwa Bunge anaitwa Sam Atandi, tuko na Mbadi kwa Treasury, saa hii mimi ndio kama leader kwa bunge ndo naangalia hawa vile wanafanya kazi, vile wanagawa mali na rasilimali za Kenya. Zamani nilikuwa naona kwa Viusasa’’

Junet amewaonya maafisa wa serikali dhidi ya kutotekeleza majukumu yao akisema watatimuliwa katika nyadhfa zao.

‘’Na Mtu yeyote ambaye atakuwa na tabia kama za Gachagua atatimuliwa tu, awe Mister, awe Deputy mwingine wembe ni ule ule tu’’