Gavana wa Kaunti ya Nakuru, Susan Kihika, na mumewe Sam Mburu, wamechapisha picha ya familia wakionesha pacha wao wanaoaminika kuzaliwa hivi karibuni, hatua iliyozima uvumi kuhusu sababu ya kuwapo kwake Marekani kwa muda mrefu.

Kihika amekuwa katika likizo ya uzazi nchini Marekani, hali ilinayoendelea kuzua mjadala kuhusu uongozi wake. Katika picha hiyo ambayo imesisimua hisia, Kihika anaonekana akiwa ameketi kwenye kiti akiwa amevalia blauzi nyeupe huku akiwabeba pacha mikononi, naye Mburu akiwa amesimama kando yake.

Baada ya picha hiyo kusambaa, viongozi mbalimbali akiwamo walituma pongezi kwa familia hiyo.

Hata hivyo, kukosekana kwa Kihika kwa muda mrefu kumezua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi, akiwamo Evans Kimori ambaye aliandika barua kwa Rais wa Marekani akitaka Kihika kurejeshwa nchini, akidai uongozi wa kaunti umedorora.

Kabla ya kufichua kuwa alikuwa likizoni kwa ajili ya kujifungua, tetesi mbalimbali zilienea mitandaoni, baadhi wakidai alikuwa kwenye shughuli za kibiashara au kisiasa, huku wengine wakihusisha safari hiyo na maandalizi ya uchaguzi wa 2027.

Kihika aliwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa Naibu Gavana David Kones anaendelea kusimamia shughuli za serikali ya kaunti kikamilifu.