YouTuber maarufu wa Marekani Mr. Beast, jina halisi James Stephen “Jimmy” Donaldson, kwa mara nyingine amedhihirisha moyo wake wa ukarimu.
Wakati huu, Beast amebadilisha maisha ya wanafunzi na walimu katika shule moja humu nchini. Katika video ambayo amechapisha kwenye mtandao wake wa YouTube, Mr. Beast amefichua ziara yake ya kushtukiza katika shule hiyo, ambapo alishangazwa sana na mazingira mabaya ya masomo.
Mwanzo, aliona watoto wameketi kwenye miamba kwa sababu ya ukosefu wa madawati, jambo ambalo lilimgusa sana.
“They have few desks in school that some of them sit on the rocks. This desk is supposed to have two pupils, not four. Something as simple as new desks, they have to sit on rocks!”Beast alibainisha kwenye video hiyo, akiwa amekatishwa tamaa na kile alichokiona.
Mara hiyo hiyo, aligeukia mwalimu na kumwambia awaulize wanafunzi hao iwapo wanataka madawati mapya. Wanafunzi hao waliitika kwa shangwe na bila kupoteza muda, lori lililojaa madawati mapya lililetwa kwenye kiwanja cha shule, na kubadilisha muonekano wa madarasa mara moja.
Beast hakumalizia hapo, baada ya kufahamu kwamba jikoni la shule lilikuwa katika hali chakavu, alifadhili ujenzi wa jikoni mpya na kuruhusu shule kuandaa chakula katika mazingira safi na salama.
Pia, alipotambua utegemezi wa shule katika kilimo kwa chakula na mapato, Mr Beast aliongoza ujenzi wa kivungulio(greenhouse) kwenye shamba la shule.
“We have built a brand-new kitchen and on top of revamping the school, we are also digging a well with water storage plus a greenhouse and a farm. We are providing this school with everything they need,”alieleza.
Ili kusaidia shule hiyo kukabiliana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi, Mr. Beast alisema wanashirikiana na mashamba makubwa kusambaza chakula huku akitoa trekta ambayo itasaidia walimu na wanafunzi hao ambao kwa sasa wanategemea kazi ya mikono(manual labour) katika kulima shamba lao.
“These farms are using manual labour and that’s not sufficient enough to produce as much food as the school need. Instead of doing manual work like this, they can use this brand-new tractor. This tractor is more important than you may realize,” aliongezea.
Aliwatunuku pia lori iliyojaa chakula kuhakikisha wanaendelea kupata mlo shuleni.
Mr. Beast amedhihirisha msururu wa matendo ya ukarimu anayoendeleza. Hapo awali, Mr. Beast alileta athari ya kudumu kwa maisha ya Wakenya zaidi ya 500,000 aliposimamia ujenzi wa visima 52 katika vijiji mbalimbali kote nchini, kuhakikisha maji safi inafikia jamii waliotatizika kuyapata. Kwa kuongezea, alitoa kompyuta kwa shule zisizojiweza.