Mama, watoto wake watatu na binamu yao, walioshtakiwa kwa kufukua mwili wa marehemu mumewe, Noah Tanui, aliyefariki miaka 15 iliyopita, wameachiliwa na mahakama ya Eldoret.
Watano hao wameamrishwa kurejea nyumbani kuzika upya mwili huo kulingana na mila za jamii ya Wakalenjin baada ya mahakama kutambua kuwa kaburi ya marehemu bado liko wazi.
Familia hiyo ilikuwa imefukua mwili wa Tanui, aliyefariki mwaka wa 2010 kutokana na mzozo wa ardhi.
Akiwasilisha ombi kwa mahakama kuachilia familia hiyo, Afisa Mkuu wa kituo (OCS) Alividza Muhoye alisema wanafamilia hao ndio watu pekee waliotakiwa kurudisha mwili huo na kufukia kaburi lililo wazi kulingana na mila za jamii zao.
Muhoye aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao walisema siku ya kukamatwa, waliamua kuufukua mwili huo ili kupata maelezo ya mgogoro wa muda mrefu wa ardhi ya familia uliokuwa ukiwakatisha tamaa.
“Your honour, I request this court to consider releasing the accused on bond since the grave that contained the remains of the late is still open and it is posing a health hazard in the area,” Alividza Muhoye aliiomba mahakama.
Hakimu Mkuu wa Eldoret Kesse Cherono aliamuru Sally Tanui (mke wa marehemu) na wanne hao waachiliwe ili wafanye ibada ya mazishi nyumbani kwao katika kijiji cha Leseru, kaunti ndogo ya Kapseret.
Mahakama iliwapa kila mshtakiwa bondi ya Ksh 500,000 au dhamana ya pesa taslimu mbadala ya Ksh100,000 kila mmoja.
Sally Tanui, mke wa marehemu, pamoja na William Cheruiyot, Abraham Kipyego, Faith Jepng’etich na Dickson Kipchirchir, walishtakiwa kwa kuufukua mwili huo bila kibali, kinyume na kifungu cha 146 (1) cha Sheria ya Afya ya Umma SURA 242.
Washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao na kesi hiyo itatajwa Aprili 28,2025.