Maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC wamevamia ofisi na makazi ya Gavana wa Kaunti ya Kiambu, Kimani Wamatangi, wakichunguza madai ya uporaji wa fedha za umma na muingiliano wa majukumu.

Viongozi wengine tisa wa kaunti hiyo pia walilengwa katika msako huo, ambapo makazi na maeneo yao ya kazi yalifanyiwa upekuzi.

Maafisa hao kumi wa umma wanaripotiwa kuwa chini ya uchunguzi kwa miezi kadhaa sasa kufuatia madai ya usimamizi mbaya wa fedha za umma katika kaunti hiyo.

Kwa muda mrefu sasa, viongozi wa kisiasa kutoka Kaunti ya Kiambu wamekuwa wakitaka uchunguzi dhidi ya Gavana Wamatangi, aliyemrithi aliyekuwa Gavana Ferdinand Waititu, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo gerezani baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ufisadi ya Shilingi milioni 588.

Ikumbukwe Februari 2024, Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa alitoa wito kwa EACC kuchunguza kuongezeka kwa kiwango cha fedha zinazotumika katika malipo ya kaunti hiyo, akidai kuwa gavana alibadilisha mfumo kutoka wa kiotomatiki hadi wa mikono.

Seneta huyo alidai kuwa mabadiliko hayo yalichangia kuwapo kwa wafanyakazi hewa, akidai kuwa kiasi cha Shilingi milioni 390 ziliibwa kupitia njia hiyo.