Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini akidai kuna jaribio la kutaka kumuua.
Katika barua aliyomwandikia Inspekta Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja Gachagua amemshtumu akidai amekataa kumpa ulinzi.
Gachagua amedai kuwa Kanja alimpokonya walinzi katika kile ambacho amesema ni njama ya kuweka maisha yake katika hatari.
Katika barua hiyo Naibu huyo wa Rais aliyetimuliwa ofisini ameorodhesha misururu ya majaribio ya vurugu zilizoshuhudiwa katika mikutano na ibada mbalimbali alizohudhuria.
Aidha ameibua madai kuwa kumekuwapo na majaribio ya kuyavamia makazi yake jijini Nairobi, Nyeri na maeneo mengine nchini na watu anaodai Kanja anawafahamu vyema.
Sio hayo tu, Gachagua anadai maafisa wa Idara ya Ujasuzi NIS wamekuwa wakimfuata mara kwa mara wakitumia magari yasiyo na nambari za usajili.
Amesema, ‘’ You are aware that there have been deliberate plans to attack my homes in Nairobi, Nyeri and my properties across the country by individuals well known to you or where you are a culpable accomplice. You are also well aware that Security Agencies have been trailing me with marked and unmarked vehicles.’’
Amesema Kenya ni nchi yenye demokrasia komavu akisisitiza ana haki kikatiba wala serikali haifai kumhangaisha ‘’ Be informed that under the Constitution of Kenya, under Chapter 4, the Bill of Rights, fundamental freedoms and rights are guaranteed to every Kenyan and not under the mercy of the State and its bureaucrats.’’
Sasa Gachagua ametoa masharti yafuatayo kwa Inspekta Mkuu wa Polisi:
i. Kukamatwa na kushtakiwa mara moja kwa wale wote waliotekeleza vitendo vya vurugu dhidi yake.
ii. Kutoa ulinzi katika mikusanyiko yote ya umma atakayohudhuria kama kiongozi wa nchi.
iii. Kumrejeshea walinzi mara moja bila kuchelewa.
iv. Kuacha mara moja kuingilia mikutano ya amani ya wananchi.
v. Kusitisha mara moja kufuatwa na kufuatiliwa na maafisa wa NIS na mashirika mengine ya usalama.
vi. Kulinda nyumba na mali yake
Amesema iwapo chochote kitamfanyia pamoja na familia yake basi Inspekta huyo Mkuu wa Polisi atawajibishwa.