Waziri mteule wa Jinsia, Hannah Wendot Cheptumo, Jumatatu tarehe 14 Aprili, 2025, alihusisha janga la mauaji ya wanawake nchini Kenya na kuwategemea mno wanaume kifedha.
Wakati wa uhakiki wake katika majengo ya Bunge jijini Nairobi, Cheptumo aliwaambia wabunge kwamba ikiwa ataidhinishwa, mojawapo ya hatua zake kuu za kushughulikia mauaji ya wanawake nchini Kenya ni kuboresha uhuru wa kifedha kwa wanawake.
“Femicide, the Intentional killing of women and girls, is brought about by dependency. If girls were able to have economic power, they would not depend on either Gender. Sometimes you find them in places where they are exposed because they are trying to have alternative source of income,” alidai Cheptumo.
Cheptumo aliendelea kuelezea kuwa atahakikisha wanawake wanapata elimu kwani mwanamke ambaye amepata elimu hatajiweka katika hali yoyote inayohatarisha maisha yake.
“We also have challenges to do with Education. If a woman is educated, chances are they will avoid some of these challenges,” Cheptumo alizidi kupigia debe mikakati atakayotumia.
Spika wa Bunge Moses Wetangula hata hivyo hakuridhishwa na mikakati hiyo ikizingatiwa kuwa wanawake ambao wamepoteza maisha yao katika nyumba za kukodi kwa muda mfupi baadhi wamesoma mpaka Chuo Kikuu.
Wetangula aliuliza hivi,”The girls who have been killed in ‘Airbnbs’ are in universities, they are educated.”
“They are educated but those ones are looking for money,” Hannah alimjibu na kuzua gumzo mtandaoni.
Hannah Cheptumo ni mjane wa marehemu Seneta wa Baringo William Cheptumo, ambaye aliaga Februari.
Yeye ni mwanasheria anayejitambulisha kama mtetezi wa haki za wanawake na haki ya kijamii.
Rais Ruto alimteua mnamo Machi kujaza nafasi hiyo, ambayo imekuwa bila waziri tangu Bunge mnamo Agosti 2024 kukataa uteuzi wa Stella Soi Lang’at.
Awali, wizara hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Aisha Jumwa na iliachwa wazi kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mnamo Julai 2024 baada ya wiki kadhaa za maandamano ya kuipinga serikali.