Bunge la Kaunti ya Nairobi limepinga vikali pendekezo la Wizara ya Afya kwamba makaburi ya Lang’ata yatafungwa kwani ni tishio kwa afya ya wananchi.

Kulingana na Bunge hilo, usimamizi wa makaburi hayo ni jukumu la kaunti wala sio Wizara ya Afya huku likitaka eneo mbadala la kuizika mili kutolewa kabla ya makaburi hayo kufungwa.

Mwakilishi Wadi wa Mountain View Mourice Ochieng, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Kaunti anasema wanajadili zaidi kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa. Ochieng’ anasema kwa siku mili ishirini huzikwa katika makaburi ya Lang’ata.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Nairobi Tom Nyakaba, anasema ni Kaunti ndiyo inayostahili kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo.

Kulingana na Kaunti, makaburi ya Lang’ata yana nafasi ya mili elfu mbili wakiitaka Wizara kutoharakisha mpango wa kuyafunga.

Wiki jana Wizara ya Afya ilitangaza kuwapo kwa mipango ya kutafuta eneo mbadala ambapo mili itakuwa inazikwa, makaburi ya Lang’ata yatakapofungwa.