Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ametishia kumwandikia Rais William Ruto kuivunja serikali ya kaunti iwapo mzozo miongoni mwa Wawakilishi Wadi utaendelea.

Akizungumza katika kipindi cha Breakfast 47, Nyaribo amesema iwapo mivutano hiyo itaathiri maendeleo ya kaunti  basi hana bundi kulivunja bunge.

Gavana huyo amewalaumu baadhi ya viongozi wa kaunti ya Nyamira akiwamo seneta Okong’o Omogeni na Mbunge Joash Nyamoko, akisema wanawachochea mvutano unaoendelea katika kaunti.

Wengine ambao amewalaumu ni wale aliowashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na wanaolenga kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Gavana ameyasema hayo huku mkanganyiko ukiendelea kushuhudiwa katika uongozi wa kaunti ambayo sasa ina mabunge mawili tofauti pamoja na maspika wao.

Bunge la kwanza ni la Enock Okero, aliyeondolewa madarakani na ambalo linafanyia vikao vyake katika maeneo manne aliyoyachagua na kuyaita ‘’Bunge Mashinani’’.

Okero alikuwa amepinga kutimuliwa kwake mahakamani.

Bunge jingine ni la Naibu Spika Thaddeus Nyabaro ambaye anafanyika vikao vyake katika bunge la Kaunti.