Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani NTSA sasa inasema angalau watu 1,139 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari 1 na Machi 31, 2025.

Idadi hii inaonesha kupungua kiasi ikilinganishwa na vifo 1,166 vilivyoripotiwa katika kipindi sawa na hicho mwaka wa 2024.

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka NTSA, waathiriwa wakuu walikuwa watu wanaotembea kwa miguu ambao ni 420, wakifuatwa kwa karibu na waendesha pikipiki 301.

Abiria walikuwa nambari tatu kwa idadi ya vifo katika kipindi hicho, wakiwa 189, huku abiria wa pikipiki (pillion passengers) waliofariki duni wakiwa 130.

Takriban madereva 83 na waendesha baiskeli 16 walifariki katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2025.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, jumla ya watu 5,856 walihusika katika ajali za barabarani katika kipindi hicho, idadi iliyopungua kwa 1,908 ikilinganishwa na mwaka jana kwa kipindi katika hicho.

Miongoni mwa waathiriwa hao, watu 3,316 walijeruhiwa vibaya huku 2,693 wakipata majeraha madogo.

Katika takwimu hizo, idadi ya abiria wa pikipiki na waendesha pikipiki imeongezeka kwa kiasi kikubwa, ishara kuwa bado kuna haja kubwa ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya usalama barabarani.

Haya yanajiri licha ya juhudi za polisi na NTSA kuweka mikakati ya kuzuia ajali zaidi kutokea.

Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kurejeshwa kwa vifaa vya kupima viwango vya pombe kwa madereva (Alcoblow) barabarani ili kudhibiti ulevi wakati wa kuendesha.

NTSA imetoa onyo kali kwa madereva kutii sheria na taratibu za usalama barabarani hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika msimu wa Pasaka, ambapo watu wengi husafiri kwenda kujumuika na familia zao.

Operesheni ya kitaifa ya kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria za usalama barabarani inaendelea, ikiwa inalenga sababu kuu za ajali kama vile ulevi miongoni mwa madereva na kutotii sheria za trafiki.