Katika Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret, zaidi ya wafanyabiashara wa ngono 4,000 wamo hatarini kutokana na uhaba mkubwa wa kondomu na dawa za kuzuia virusi vya Ukimwi kabla ya mtu kuambukizwa (PrEP). Uhaba huu umetikisa huduma muhimu za afya katika maeneo ya Mai Mahiu, Longonot, Naivasha, Gilgil, Kikopey, Pipeline, Salgaa na Sachangwan.

Barabara hiyo kuu si tu njia ya usafiri, bali pia ni eneo la mwingiliano mkubwa wa watu kutoka Kenya na mataifa jirani kama Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi. Wafanyabiashara wa ngono wengi hupata wateja kutoka kwa madereva wa malori wa safari za masafa marefu, hali inayoongeza uwezekano wa kusambaa kwa maambukizi ya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.

Kwa sasa, huduma bila malipo katika vituo vya afya zilizokuwa zikiyalenga makundi maalum kama wafanyabiashara wa ngono zimesimama kwa sababu ya uhaba huu.

Baadhi ya wanawake wanaofanya biashara hiyo wanaelezea hofu ya afya yao. Hali hii imezua taharuki pia kwa wanaharakati wa afya ya umma.

Afisa wa afya wa Kaunti ya Nakuru, Roselyn Mungai, alithibitisha kuwa changamoto hiyo inatokana na kujiondoa kwa shirika la USAID, ambalo lilikuwa likifadhili miradi mingi ya afya, ukiwamo usambazaji wa kondomu na dawa za PrEP.

Wakati huo huo, Dkt Reuben Osiemo wa NASCOP aliwahimiza washikadau kuweka juhudi za pamoja ili kuhakikisha kondomu zinapatikana tena kwa urahisi.

Kenya huhitaji zaidi ya kondomu milioni 400 kwa mwaka, lakini serikali husambaza karibu nusu tu.