Maafisa wa Upelelezi Mtaani Kasarani wamewatia mbaroni wanaume wawili waliokuwa wakitekeleza ulaghai mtandaoni kwa kujifanya wanawake warembo wanaotoa huduma za “kukanda kitaalamu”, (professional massage).

Watuhumiwa hao, Alex Mugo Wachira na Simon Chomba Mbogo, walikuwa wakiwanasa wateja kupitia matangazo ya huduma hizo mtandaoni.

Mmoja wa waathiriwa, aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kasarani. Alivutiwa na tangazo lililodai kwamba wanawake warembo wawili walikuwa wakitoa huduma za kiwango cha juu, na akaelekezwa kwenye makazi yao katika eneo la Lumumba Drive, Kasarani.

Lakini dakika chache baada ya kuanza ‘kukandwa’, mambo yalibadilika ghafla. Wawili hao walitoa visu na kufichua sura zao halisi hawakuwa na ujuzi wowote wa kuwakanda watu kitaalam. Walimlazimisha mteja kuwatumia Shilingi 280,000 kwa nambari ya simu yao na kumpora mali nyingine kabla ya kumtupa nje kwa fedheha.

Uchunguzi ulianzishwa, na kupitia mbinu za kiteknolojia, wawili hao walikamatwa wakiwa wakivinjari katika eneo la Kamiti prison, ikiaminika huenda walikuwa wakitumia fedha za wizi huo.

Kwa sasa wanazuiliwa na wanaendelea kuhojiwa wakisubiri kufikishwa mahakamani.