Maafisa wa polisi Mjini Kitui, wanachunguza kisa ambapo mguu wa binadamu umepatikana katika shimo la kutupa taka, katika eneo la Site mjini humo.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Kitui ya Kati Peter Karanja, amesema baada ya kupokea ripoti kutoka kwa wakazi, maafisa wake wamefika katika eneo la tukio na kupata mguu huo umefungwa kwa karatasi, kuashiria huenda ulikatwa kwa njia ya upasuaji.

Aidha kwenye harakati za kuchunguza chanzo cha kupatikana kwa mguu huo, wamepokea ripoti kutoka kwa Afisa wa Afya ya Jamii, katika eneo la Kitui ya Kati Festus Kilunda ambaye amethibitisha kuwa mguu huo huenda ni wa mgonjwa aliyekuwa akitibiwa.

Kamanda huyo ameelezea kuwa mguu huo ulikuwa umeanza kuoza.

“Hicho kiungo, kimetupwa kinyume na desturi za Jamii,na ni hatari kwa afya ya wakazi wa eneo hili. Hatujapata ripoti yoyote hivi karibuni kutoka kwa hospitali hapa Kitui kuhusiana na mtu kukatwa mguu, labda imetoka kwa hospitali mbali na Kitui na ikatupwa hapa.” aliongezea

Amewarai wakazi katika eneo hilo, kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kutoa taarifa ili kusaidia katika uchunguzi.

Ni tukio ambalo limewachangaza wakazi wa eneo hilo, wakisema ni mara yao ya kwanza kuona sehemu ya kiungo cha mwili wa binadamu kutupwa karibu na makao yao.

Maafisa wa polisi wameuchukua mguu huo na kuupeleka katika Hifadhi ya Maiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Kitui huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini kama ni madaktari walihusika au ni tukio la uhalifu.

Written by, Raphael Mulatya