Takriban watoto 45,000 nchini huenda wakakosa makao kufuatia mpango mpya wa serikali wa kufunga zaidi ya makao 1,000 ya watoto, ili kuwezesha mfumo mbadala wa malezi ya kijamii na kifamilia.

Serikali kupitia Baraza la Kitaifa la Huduma za Watoto imeanzisha mageuzi makubwa katika utunzaji wa watoto, kwa lengo la kuhamisha watoto kutoka katika makao ya malezi na kuwaweka katika mazingira ya familia au jamii.

Kwa miaka mingi, watoto waliotelekezwa au yatima wamekuwa wakihifadhiwa katika makao maalum kote nchini, lakini sasa serikali inataka wahudumiwe ndani ya familia kwa mujibu wa Sera ya Kitaifa wa Utunzaji wa Watoto ya mwaka 2022-2032.

Kupitia taarifa rasmi, Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza hilo, Adanoor Mohamed, alisisitiza kuwa utafiti umebainisha kuwa malezi ya kifamilia yana manufaa zaidi kwa ustawi wa mtoto ikilinganishwa na makao rasmi.

Taarifa hiyo imetumwa kwa makamishna wa kaunti, maafisa wa ustawi wa jamii, viongozi wa masuala ya watoto katika kaunti, pamoja na washikawadau wengine muhimu katika sekta hiyo.

Kulingana na takwimu rasmi, kuna makao 902 yanayowatunza watoto 44,070 na taasisi 30 za serikali zinazowahudumia watoto 1,443 kote nchini.

Mpango huu ni sehemu ya ahadi ya Kenya kutekeleza ajenda ya kimataifa ya kuondoa mfumo wa makao ya watoto kama ilivyoainishwa kwenye Kongamano la Watoto la mwaka, 2024. Mfumo huo pia unajikita katika kuimarisha familia ili kuzuia utengano.

Hatua hii ni mabadiliko makubwa katika historia ya utunzaji wa watoto nchini, huku serikali ikiwataka washikadau wote kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mabadiliko haya yanafanikiwa kwa manufaa ya watoto wote walio katika mazingira hatari.