Je, katika uhalisia wa maisha yako unaweza kula kiasi kipi cha chapati? Shindano la kula chapati Mjini Busia litakushangaza.

Wanaume wawili mjini Busia wameushangaza umati baada ya kila mmoja kula chapati 24 wakati wa shindano la aina yake liliofanyika katika eneo la kuyakarabati magari mjini Busia.

Ni shindano lililomkutanisha gwiji tajika wa kurarua chapati mjini Busia Godfree na mwenzake anayetesa katika jiji la Kisumu Henry Otieno na kushuhudiwa na makumi ya wakazi ambao walisalia vinywa wazi.

Imeelezwa kuwa shindano liliandaliwa na baadhi ya wahudumu wa eneo hilo ili kupima uweledi wa Godfree Okumu ambaye amekuwa na sifa ya kula chapati kati ya 15-20 pamoja na maharagwe ya shilingi themanini kila siku katika hoteli za mji huo wa mpakani suala ambalo limewachochea wenzake kumsaka mpinzani.

Na baada ya wiki kadhaa, walimpata mpinzani kwa jina Henry Otieno ambaye ni muhudumu wa kubeba mizigo jijini Kisumu ambapo baada ya kukamilika kwa maandaliza ya mchuano huo, Otieno alisafirishwa hadi mjini Busia tayari kwa shindano.

Kwenye shindano hilo lililofanyika tarehe 15 ya mwezi huu wa Aprili washiriki wote wawili waliandaliwa chapati 24 kila mmoja huku Okumu mwakilishi wa mji wa Busia akianza kwa vishondo kwa kuteremsha vipande vya chapati zake lita moja, maji kisha kuongeza mkate gramu 400 na kumaliza mpinzani wake akisalia na chapati mbili.

Hata hivyo, kwa kuwa kutangulia kwa baa sio dhihirisho la kulewa, Okumu alivuliwa ushindi baada ya kutapika na kumpisha mwenzake Otieno kunyakuwa ushindi baada ya kukamilisha chapati zake 24 salama.

Wananchi mjini wamewasifia wawili hao na kuiomba serikali kuweza kuwatambua miongoni mwa watu wenye vipaji vya kipekee.

Aidha wamemtaka mwakilishi wao Godfree Okumu kufanya mazoezi ya ziada kabla ya kuingia kwenye shindano lingine na mshiriki kutoka taifa jirani la Uganda.

Written by, Seth Ngero