Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungw’a ameitaka jamii ya Maa kutokubali siasa za aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, wakimshtumu kwa kueneza uongo.
Kimani ambaye aliandamana na viongozi wengine ameshtumu ziara ya hivi punde ya Gachagua katika eneo la Kajiado akisema hakuwapelekea suluhu yoyote, bali lengo lilikuwa kuwachochea wakazi kumpinga Rais William Ruto waliyesema anawahudumia wananchi.
Wakizungumza katika hafla iliyoandaliwa na Mwakilishi wa Kike wa Kajiado Leah Sankaire viongozi hao wmewakosoa wenzao wa amii hiyo ya Maa wanaomuunga mkono Gachagua wakisema wanaipotosha jamii.
Ichungw’a alisema, ”Wakisema ya Ruto, Ruto si agenda ya mwananchi wa Kajiado, mtu akikuja kupiga siasa Kajiado aje akutajie maendeleo ya mwananchi ambayo ni agenda yake na manifesto yake.”
Naye Mbunge wa Kajiado Central Memusi Kanchory amewashauri wananchi kuwapigia kura viongozi wanaofanya maslahi yao kipaumbele. Alisema, ”Na mimi nataka niwaambie, mnapenda wanasiasa wakiwachekesha lakini nyinyi ndio mnachagua hao watu ambao wanakuja kuwadhulumu. Mimi nataka kila kiongozi kwa nafasi yake akirudi akitafuta kura, muulize ni nini umetufanyia.”