Maafisa wa usalama katika eneo la Rongo wameanzisha uchunguzi kufuatia kifo cha kutatanisha kilichoripotiwa katika Kanisa la St. Joseph Missions of Africa ililoko kijiji cha Kochola, eneo la Kanyadiedo.
Mwili wa mwanaume mmoja aliyetambuliwa kama Francis Muli ulipatikana ndani ya chumba cha maombi, ukiwa umevalishwa nguo jeupe na kufunikwa kwa shuka la kijivu. Mwili huo ulikuwa na majeraha usoni na povu lilikuwa likitoka mdomoni.
Ripoti ilitolewa Jumatatu jioni na Naibu Chifu wa eneo hilo, Abiud Rariende. Kamati ya Usalama na Ujasusi ya Kaunti Ndogo, ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti na polisi, walifika katika eneo la tukio, lililo takriban kilomita 10 kutoka Kituo cha Polisi cha Rongo. Mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Rosewood ukisubiri kufanyiwa upasuaji.
Mapema Jumatatu, mwili mwingine pia ulikuwa umeripotiwa kupatikana katika eneo ilo hilo.
Katika msako uliofuata ndani ya kanisa hilo, maafisa wa usalama waliwaokoa watu 57 waliokuwa wakiishi humo. Waliokolewa walikuwa na kati ya umri wa miaka 18 na 75.
Baadhi yao walionekana wanyonge. Walikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Rongo kwa uchunguzi wa kiafya, lakini walikataa kabisa kupimwa na badala yake walianza kuimba nyimbo za kidini kwa sauti, wakivuruga utulivu wa hospitali.
Hatimaye waliondolewa na kupelekwa katika kituo cha polisi kusubiri maelekezo zaidi. Idara ya Upelelezi DCI Rongo imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.