Maafisa wa Polisi katika eneo la Pkokot Magharibi wanachunguza mauaji ya kikatili ya mwanaume katika Klabu ya Regency Jumanne usiku.
Polisi wanasema mwanaume huyo ambaye ametambuliwa kwa jina Peter Ngoriana wa umri wa miaka hamsini alivamiwa alipokuwa akivinjari katika klabu hiyo mwendo wa saa mbili usiku. Mshukiwa wa mauaji Benjamin Limakwang na ambaye mlinzi katika kituo cha Huduma Centre katika eneo hilo, anasemekana kumvamia marehemu kwa panga kisha kumkatakata.
Uchunguzi wa awali wa polisi unaonesha kuwa huenda mauaji hayo yametokana na mzozo wa kimapenzi baina ya wawili hao. Inadaiwa marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mshukiwa.
Mkuu wa Idara ya Upelelezi Daniel Musangi amesema mshukiwa alitoweka baada ya mauaji hayo na anaendelea kutafutwa.
Mwili umepelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Kapenguria.