Athari za mvua kubwa inayoendelea kunyesha zinazidi kushuhudiwa huku watu sita wakiripotiwa kufariki na wengine kuachwa bila makao kufuatia mafuriko jijini Nairobi.

Polisi wanaonya kuwa huenda idadi ya waliofariki iakongezeka kwani watu wengi hawajulikani waliko ikihofiwa kuwa huenda walisombwa na maji.

Miongoni mwa waliofariki ni mama na wanawe wawili baada ya kuangukiwa na mawe makubwa yaliyobebwa na maji nyumbani kwao katika mtaa wa Mathare 4A.

Kamanda wa polisi jijini Nairobi George Sedah amewashauri watu wanaoishi katika maeneo hatari kuhamia yale yaliyo salama.

Katika tukio jingine la kusikitisha, mtu mmoja amefariki dunia katika mtaa wa Mukuru kwa Reuben baada ya kusombwa na mafuriko. Polisi wanasema takriban watu mia tano katika mtaa huo wameachwa bila makao

Aidha mili mingine miwili imepatikana katika maeneo tofauti jijini. Mwili mmoja umepatika kando ya Mto Ngong’ katibu la kivukio cha Likoni mtaani South B huku mwingine ukipatikana katika Barabara ya Jogoo. Mili hiyo inaaminika kusombwa na mafuriko.

Tayari maafiwa wa vitengo mbalimbali wameanza kuwahamisha wakazi wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na athari ya kukumbwana mafuriko.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi imewatuma maafisa wake nyanjani kufuatilia hali na kudhibiti hali.

Ikumbukwe Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ilikuwa imeonya kuwa mvua kubwa itanyesha katika maeneo mbalimbali nchini wiki hii.