Katika hali ya maelewano ya pamoja na kujitolea kwa dhati kutatua mzozo kwa njia ya amani, Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya DRC na waasi wa M23 wamekubaliana kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo huku wakianza mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo wa muda mrefu.
Haya yameafikiwa wakati wa mazungumzo yaliyoongozwa na Serikali ya Qatar.
Baada ya majadiliano ya wazi, pande zote mbili zimekubaliana kuchukua hatua kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa mipango iliyopo.
Pande zote mbili sasa zimethibitisha tena kujitolea kwao kusitisha mapigano mara moja, kuacha vitisho na chuki vile vile kuzitaka jamii zote za eneo hilo kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo.
Aidha pande hizo zimekubaliana kuendeleza makubaliano hayo kama msingi wa mazungumzo ya kina yatakayolenga kurejesha amani ya kudumu nchini Congo. Mazungumzo hayo yatachunguza sababu kuu za mzozo unaoendelea pamoja na njia bora za kumaliza mapigano katika eneo la Mashariki ya DRC.
Wawakilishi wa DRC na M23 wamekubali kutekeleza mara moja makubaliano hayo katika kipindi chote cha mazungumzo hadi yatakapokamilika.
Aidha, pande zote zimewaomba wananchi wa Congo, viongozi wa kidini na vyombo vya habari kuunga mkono na kueneza ujumbe huo wa matumaini na amani.
Wakati uo huo, DRC na M23 wameishukuru Serikali ya Qatar kwa juhudi zake na kujitolea kwa hali ya juu katika kuratibu mazungumzo hayo ya amani, ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kukuza maelewano baina ya pande zinazohusika.