Viongozi wa Kenya Kwanza wameitetea ziara ya Rais William Ruto nchini Uchina na kuwakashfu wanaoikosoa. Wakizungumza Jumapili wamesema ziara hiyo haikuwa ya kutafuta madeni bali kuwavutia wawekezaji.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah amesema wawekezaji hao watasaidia kufanikisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara.

Ichung’awah alisema ‘’Rais hajaenda Uchina kukopa, ameenda kutafuta wawekezaji.’’

Kulingana na Ichung’wah miradi mingi mikubwa mikubwa nchini imefanikishwa na wawekezaji wa nje akitoa mfano wa Barabara Kuu ya Thika iliyojengwa wakati wa utawala wa Hayati Rais Mwai Kibaki.

‘’Vile Thika Road ilijengwa na mheshimiwa Mwai Kibaki ikafungua sehemu ya Thika, ikafungua Murang’a, ikafungua Nyeri, pia Rais William Ruto atawajengea hii Barabara ya Rironi ifike Malaba, ifungue sehemu hii uchumi wenu uweze kupanuka kama sehemu nyingine.’’ Alisema Ichung’wah.

Kauli hiyo ya Ichungwah pia imesisitizwa na Kiranja wa wengi katika Bunge hilo la Kitaifa Silvanus Osoro. Mbunge huyo wa Mugirango Kusini amewashtumu vikali wale wanaolalamikia ziara hiyo ya Rais akisema hawaelezi manufaa yake.

Osoro alisema hivi ‘’ Last week ame-sign deals na investors wanakuja ku-invest hapa pesa nyingi. Tena niwaona wakisema mbona Rais ameenda kutafuta wachina si angetafuta Wakenya. Mnataka nini?’’

Wakati wa ziara yake nchini Uchina mapema wiki jana, Rais Ruto alitia saini mikataba ishirini na mawili ya ushirikiano baina ya mataifa haya mawili.

Aidha Rais alifanikiwa kupata mkopo wa shilingi bilioni 126 ambazo zitatumika kufanikisha miradi mbalimbali.

Miongoni mwa miradi mikuu inayofanikishwa kwa ushirikiano na serikali ya Uchina ni ujenzi wa reli ya Kisasa SGR.