Waziri wa Usalama, Kipchumba Murkomen, atafanya mkutano wa usalama na maafisa wakuu wa serikali katika eneo la Bonde la Kerio Jumatatu, Aprili 28, 2025. Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha amani katika eneo hilo ambalo limekumbwa na tatizo la utovu wa usalama kwa muda mrefu. Mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Chesongoch Sisters kilichoko Kaunti ya Elgeyo Marakwet, utawakutanisha viongozi wa ngazi za juu za kiusalama na Maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAOs) kutoka maeneo ya Marakwet Mashariki, Baringo Magharibi, Tiaty, Bonde la Kerio na Pokot Kati.

Mkutano huo unajiri wakati ambapo Operesheni Maliza Uhalifu (OMU), iliyoanzishwa mwaka 2023 ili kukabili uhalifu na utekaji nyara katika eneo la Kaskazini mwa Bonde na Ufa, inaendelea kupata mafanikio makubwa. Awamu ya kwanza ya operesheni hiyo imesaidia kurejesha shughuli za kiuchumi, shule kufunguliwa, hospitali, na kutekelezwa kwa miradi ya kuimarisha miundombinu muhimu katika maeneo yaliyoathirika.

Aidha kufunguliwa kwa kituo cha pili cha kiusalama katika eneo la Kirimon, Kaunti ya Laikipia, ni sehemu ya juhudi za serikali kukabili kabisa uhalifu katika maeneo hayo. Kituo hicho kipya kinajumuisha kituo kilichoko Chemolingot na kinawahudumia hadi wakazi wa Laikipia, Samburu, Isiolo, na sehemu za Meru.

Mkutano wa usalama wa Bonde la Kerio pia unafuatia vikao vya Jukwaa La Usalama vilivyofanikiwa katika maeneo ya Pwani na Lower Eastern, ambapo masuala ya usalama na utoaji wa huduma yalijadiliwa kwa kina. Sasa lengo kuu la Mkutano wa Kerio litakuwa marekebisho ya muhimu katika mpango wa huduma za maafisa wa Akiba NPR, ambapo mabadiliko yatakayoangaziwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mpango wa wazi wa kutoa amri, kuimarisha usajili wa maafisa hao, kuboreshwa kwa huduma za NPRs na vifaa, pamoja na mpango wa mafunzo ya kina. Lengo ni kuhakikisha kuwa NPRs wanafanya kazi chini ya mpangilio wa amri ulio wazi na kuisaidia Idara ya Polisi na maafsia wa taasizi za kitawala NGAOs katika maeneo yaliyoathirika na ukosefu wa usalama.

Pendekezo lingine muhimu linalotarajiwa kujadiliwa ni utoaji wa leseni kwa Wakuu wa Vijiji kumiliki silaha katika maeneo yanayokabiliwa na athari kubwa ya usalama. Pendekezo hlimeungwa mkono na Waziri Murkomen ambaye anasema ni njia ya kuongeza usalama, ambapo Wakuu wa Vijijiji ambao wamepata mafunzo ya kijeshi na ambao usalama wao uko hatarini, wataruhusiwa kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda na kudumisha amani katika maeneo yao.

Pia, Waziri Murkomen anatarajiwa kushinikiza mageuzi ya kiutawala, ikiwa ni pamoja na utoaji wa zawadi, mapendekezo ya nyongeza ya mishahara, na vifaa bora kwa maafisa polisi, Wakuu wa Vijiji na wasaidizi wao. Mageuzi haya yanakusudia kuboresha ari ya maafisa wa usalama wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

Pia Waziri Murkomen anatariwa kusisitiza ushirikiano wa karibu na wabunge ili kutumiamgao wa fedha wa (NG-CDF) katika ujenzi na uboreshaji wa ofisi za NGAO.

Murkomen alisema “Waathirika wa mageuzi haya yote ya usalama ni wananchi ambao watakuwa na uwezo wa kuendelea na shughuli zao na kuwatunza watoto wao kwa amani.”