Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya ametangaza kuwa atakuwa debeni mwaka 2027.

Kupitia mitandao yake ya kijamii Jumatatu tarehe 28, Aprili Salasya amesema hatua yake inafuatia majadiliano na tafakari ya kina kuhusu hali ya taifa.

Kujitosa kwa Salasya katika kinyang’anyiro cha urais kunaibua mjadala kuhusu iwapo atakuwa miongoni mwa viongozi vijana watakaowatoa kijasho vigogo wa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.

Salasya amesema , “This decision is not made lightly,”  akisisitiza, “It is born out of a profound desire to offer bold, transformative leadership that will reposition our great nation for industrial growth, economic empowerment, and social justice.”

Mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa kwanza alikosoa mwelekeo wa sasa wa uchumi wa Kenya, akilalamikia hatua ya Wakenya wenye ujuzi kwenda mataifa ya nje kutafuta ajira ilhali maarifa yao yanahitajika kuliendeleza taifa. Alielezea maono yake makubwa yaliyojikita katika viwanda na uvumbuzi akivitaja kuwa nguzo kuu za kubuni nafasi za kazi.

Salasya amesema atatangaza chama atakachosimama nacho baadaye.

Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 35 alitoa mwaliko wazi kwa Wakenya, hasa vijana na wanawake, kuungana naye katika kile alichokiita safari kuelekea taifa jipya lililostawi.

Alisema hivi, “Together, we can and we shall build a prosperous, inclusive, and united Kenya.”

Tangazo la Salasya japo halijachukuliwa kwa uzito linaweza kuzua mjadala mkali wa kisiasa nchini.

Huku kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, zikianza kupamba moto tangazo la Salasya linaweza kuvutia umakini mkubwa, hasa kutoka kwa wapiga kura vijana wanaotaka uongozi mpya na mawazo mapya.