Mwanaume mmoja wa umri wa makamo katika kijiji cha Chesingoro katika eneo la Kusumek, Kaunti ya Kericho, anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Litein kwa tuhuma za kumbaka mpwa wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kwa mujibu wa Naibu Chifu wa eneo hilo, Alfred Korir, mmshukiwa ambaye ametambuliwa kama Justice Kipsigei Cheruiyot, alinaswa kwenye tukio hilo chumbani mwake. Inadaiwa alitekeleza unyama huo wakati mama wa mtoto alikuwa ametoka nje kufanya shughuli nyingine za nyumbani .

Mama wa mtoto pamoja na wanakijiji walimsikia mtoto akilia kwa uchungu, na walipochunguza, walimfumania mtuhumiwa ndani ya chumba hicho.

Wananchi waliokuwa na hasira walimpiga kabla ya kumkabidhi kwa maafisa wa polisi.

Mtoto huyo alikimbizwa katika hospitali ya Kapkatet na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho kwa matibabu maalum.

Korir ametoa wito kwa wazazi kuwa waangalifu na kuepuka kuwaacha watoto wao wadogo mikononi mwa watu hata kama ni wa familia, akionya kuwa vitendo vya unyama vinaweza kutokea kutoka kwa wale wanaoaminika zaidi.