Wakulima katika maeneo ya Ndii na Manga mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta wanaendelea kukadiria hasara baada ya punda milia ambao wameishi na jamii kwa zaidi ya miaka miwili kugeuka na kuwa kero kubwa.

Punda milia hao wameanza kuharibu mimea hasa mahindi huku wakiwa hatari kwa wanafunzi wanapoenda na kutoka shuleni.

Licha ya punda milia hao kuonekana kuwa kivutio cha utalii hasa kwa wanaotumia Barabara Kuu ya Nairobi-Mombasa, wakazi wa miji ya kibiashara ya Manga, Manyani na Ndii wanakadiria hasara na kuhangaishwa na wanyama hao ambao wameweka makao katika maeneo ya watu badala ya kurejea katika mbuga ya Wanyama.

Wakazi hao wanalalamikia kutowajibika kwa wafanyikazi wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori KWS.

“Hawakua hapa kutoka kitambo, kuna muda wanakujaga na wanapotea tena, hatujui ni nini inawafukuzaga kutoka huko mbugani kukuja huku, kwa sababu wakija huku, tunaita watu wa ‘kws’ wanatuambia ‘hawa si wanyama wa kutuitia’ na  wanaondoka bila kuchukua hatua yoyote”. Alilalamika Alex Kituku.

Wakazi wa eneo la Ndii wakieleza punda milia hao walianza kujitokeza kwenye miji yao ya kibiashara baaada ya ujenzi wa Reli ya kisasa SGR kukamilika mwaka 2017.

“Ni wanyama waliokuja, tuseme miaka miwili mitatu iliyopita, tuseme tangu hii sgr ndio wamepita pande hii, uharibifu wa hawa wanyama ni kutuharibia mimea na kukula chakula kama mahindi yanayoanza kukomaa” alieleza Evans Mwandawiro

Wanawake vilevile wanalalamikia usalama wao wakisema punda mlia hao ni hatari kwa usalama na maisha ya wanao wadogo hali ambayo imewalazimu kuwa makini zaidi hasa wanapoenda na kutoka shuleni na madukani.

“Kama ni usiku, umewafukuza usiku wakuja kwa shamba wamekula mahindi kama ni pojo wamekula pojo, si ati vile umewafukuza vile wameenda, utatoka kwa shamba ukirudi wamerudi, n asana sana wamekua tishio kwa watoto wetu kuenda na kutoka shuleni lazima uwe makini sababu wanaranda randa kila wakati. Alieleza Violet Anami.

Aidha, wenyeji hao sasa wanatoa wito kwa serikali na wizara zinazohusika kuchukua hatua za kufanikisha kuwarejesha mbugani wanyama hao.

Written by, Julius Mariki