Washukiwa wanne; wakiwamo raia watatu wa kigeni na Mkenya mmoja wamepigwa faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa siafu.
Wakiwa mbele ya Hakimu Anjela Njeri washukiwa David Lornoy na Seppe Lodewijckx wa Balgeria, Duh Hung Nguyen wa Vietnam na Mkenya Dennis Nganga walikiri mashtaka dhidi yao katika Mahakama ya JKIA.


Washukiwa wanasemekana kupatikana na siafu elfu tano zenye thamani ya shilingi milioni moja, katika jumba kimoja mjini Naivasha. Mahakama imesema washukiwa hao hawakuwa na kibali cha kuuza wadudu hao nje ya nchi hali inayokiuka sheria za utunzaji wa wanyama pori.
Kulingana na mlalamishi ambaye ni Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori KWS ni kwamba washukiwa hawakuwa na idhini ya kuwakusanya wadudu hao hali inayoweza kuathiri mazingira.
Washukiwa waliiambia mahakama kwmaba hawakujua kuwa walikuwa wanakiuka sheria na kuomba msamaha.
Hata hivyo, mahakama iliwapiga faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja jela ikisisitiza kujitolea kwa Kenya katika kuyalinda mazingira.