Watu wasiopungua kumi na wawili wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Alhamisi jioni katika eneo la Arimi, Barabara ya Njoro-Molo. Ajali hiyo ilihusisha gari la abiria la kuwabeba watu kumi na wanne na lori.
John Mureithi, ambaye alikuwa akisafiri kwa lori kutoka Nyahururu kuelekea Molo, alielezea tukio hilo la kutisha. “Tuliona matatu kutoka mbali ikiwa imepasuka tairi. Dereva alipoteza mwelekeo na kugongana ana kwa ana na lori letu,” alisema Mureithi. Alinusurika bila majeraha, lakini dereva wa lori alijeruhiwa vibaya.
Maafisa wa kutoa huduma za dharura na Mwakilishi Wadi wa Elburgon, Njuguna Mwaura, walifika haraka katika eneo la tukio. Abiria kadhaa waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Molo kwa matibabu.
“Hii ni jioni ya majonzi,” alisema Njuguna. “Matatu imeharibika. Nimehesabu miili kumi, ikiwamo ya mwanafunzi wa shule ya upili aliyepatikana ndani ya mabaki ya gari.”
Ripoti za awali zinaeleza kuwa huenda breki za gari hiyo ya abiria zilifeli gurudumu likapasuka nhali iliyosababisha dereva kupoteza mwelekeo kwenye mteremko na kugongana na lori lililokuwa linakuja upande wake.
“Mgongano ulikuwa mkali kiasi kwamba baadhi ya miili ya abiria iliharibika vibaya,” aliongeza Njuguna. Shirika la Msalaba Mwekundu lilishiriki katika shughuli ya kuwaokoa manusura na kutoa miili kutoka kwenye mabaki ya magari.
Njuguna alilaumu hali mbaya ya barabara kwa kuchangia ajali hiyo. “Sehemu hii ina miteremko na kona kali bila alama za tahadhari. Pia kuna mashimo mengi ambayo ni vigumu kuyaepuka ukiwa na mwendo wa kasi,” alisema. Alitoa wito kwa Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini -KeNHA kuangalia upya muundo wa eneo hilo na kufanya ukarabati ili kuepusha ajali zaidi.
Miili ya waliofariki imesafirishwa hadi Hifadhi ya Maiti ya Kaunti Ndogo ya Molo huku uchunguzi wa ajali ukiendelea.