Mahakama Kuu imekataa ombi la kutaka kesi za utekaji nyara na kupotea kwa watu kiholela nchini zipelekwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC. Katika uamuzi ambao umetolewa Ijumaa 9, Mei, 2025 mahakama imesema taasisi za humu nchini zina uwezo wa kushughulikia masuala kama hayo.

Mahakama hiyo aidha imeamua kuwa masuala ya watu kujeruhiwa anapokuwa chini ya polisi au maafisa wa polisi wanapokuwa kazini, kisheria; yanastahili kushughulikiwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Utendakazi wa Maafisa wa Polisi IPOA.

Imesisitiza kuwa hakuna taasisi nyingine miongoni mwa zile za usalama zilizo na majukumu ya kushughulikia suala kama hilo.

Mahakama pia imefanya uamuzi kuwa visa vya utekaji nyara na kutoweka kiholela kwa watu ni miongoni mwa makosa ya jinai japo imekataa kukubali ombi kwamba kesi hizo zishughulikiwe na Mahakama ya ICC ikisema taasisi za humu nchini hazijashindwa kulishughulikia suala hilo.

Jaji Lawrence Mugambi amesema hakuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa taasisi za humu nchini zimeshindwa kushughulikia visa hivyo.

Katika uamuzi wake Jaji Mugambi amesema maafisa hawawezi kujichunguza ndio maana zipo taasisi huru zilizopewa jukumu hilo.

Walalamishi katika kesi hiyo waliowakilishwa na mawakili John Khaminwa na John Mwariri kutoka Kituo cha Sheria, hata hivyo wamesema watakata rufaa kuhusu uamuzi huo.

Katika kesi hiyo, Kituo Cha Sheria, Haki Afrika, na Charles Njue walikuwa wamewasilisha kesi mahakamani wakitaka mahakama kuishinikiza serikali kuziwasilisha kesi za utekaji nyara na kupotea kwa watu kiholela katika mahakama ya ICC.