Mtazamo kuhusu jinsi lishe duni, udhaifu wa usimamizi wa viwango vya vyakula, na ulaji wa vyakula vilivyosindikwa unavyotishia kwa kimya ukuaji wa idadi ya watu na afya ya uzazi nchini Kenya.
Nilipokuwa mtoto, baba yangu alikataa kabisa kunywa soda au juisi zilizotengenezwa viwandani, isipokuwa zile zilizopatikana moja kwa moja kutoka kwa matunda safi yaliyopondwa. Alikuwa na msimamo thabiti kwamba bidhaa zenye viambato vya kuongeza muda wa matumizi au visivyoeleweka ni hatari kwa afya na hazifai kuaminiwa.
Mtazamo huu unaangazia ukweli muhimu kuhusu ufuatiliaji wa ubora wa chakula ikiwa huwezi kuthibitisha kilichomo, basi wateja hawatakuwa na imani nacho.
Kauli hii huwa na uzito zaidi tunapotathmini jinsi lishe inavyoathiri ukuaji wa idadi ya watu. Lishe duni haidhuru tu afya ya mtu binafsi, bali pia hudhoofisha afya ya uzazi na hatimaye mustakabali wa taifa. Masuala kama vile kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa, matatizo ya kutopata watoto, na kuathirika kwa afya ya uzazi miongoni mwa wanaume yamekuwa ya kawaida.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kupungua kwa uwezo wa kupata watoto hubadilisha muundo wa idadi ya watu na huongeza mzigo kwa wanaotegemea idadi ya watu, jambo linalozuia ustawi wa kiuchumi. Afya duni ya uzazi huathiri jamii kwa ujumla.
Nilishuhudia hali hii kwa macho yangu nilipokuwa nikitembea na mama yangu katikati ya jiji la Nairobi. Tulipita eneo moja maarufu ambako wanaume hukusanyika kunywa “Uji Power,” uji wa kienyeji ulioandaliwa kutokana na nafaka ya kiasili na ambao hauna viambato vya kisasa.
Mama yangu alitoa maoni kwamba huenda wengi wa wanaume hao walikuwa wanakabiliwa na changamoto za ukupungua kwa nguvu za kiume changamoto zinazochangiwa na lishe duni na kutegemea sana vyakula vilivyosindikwa.
Aidha, nilipokuwa nikifanya kazi ya usafirishaji wa bidhaa, niligundua kuongezeka kwa maagizo ya bidhaa za kuongeza nguvu za kiume. Mwelekeo huu ulionesha wazi kuwa wanaume wengi walikuwa wakitafuta suluhu kwa matatizo ambayo chanzo chake kinaweza kuwa lishe duni.
Kuzingatia ubora wa chakula na kuhakikisha lishe bora si masuala ya afya tu, bali ni masuala yanayohusu moja kwa moja na mustakabali wa taifa kwa ujumla. Kupatikana kwa chakula salama, chenye virutubisho vya kutosha na visivyo na kemikali hatarishi hakupaswi kuachwa katika mtazamo wa afya peke yake, bali pia litazamwe kama sera ya kitaifa ya idadi ya watu.
Utafiti wa kisayansi unaunga mkono hali hii. Utafiti wa mwaka 2023 uliochapishwa katika jarida la Human Reproduction Update uligundua kuwa idadi ya mbegu za kiume duniani imeshuka kwa zaidi ya asilimia 50 katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Lishe duni, sumu kutoka kwenye mazingira, na ongezeko la matumizi ya kemikali bandia vimetajwa kuwa sababu kuu.
Ingawa KEBS ina jukumu muhimu katika kusimamia viwango vya chakula, jukumu hilo halipaswi kuachiwa shirika hilo pekee. Kama watumiaji, tunapaswa kuwa waangalifu tusome lebo za chakula, tuhoji asili ya viambato, tuunge mkono masoko ya vyakula vya asili, na tuwajibishe wasambazaji. Uangalizi wa pamoja unaweza kulazimisha makampuni na mashirika kuweka viwango bora na thabiti vya ubora wa vyakula.
Kwa hivyo, ufuatiliaji wa ubora wa chakula na lishe bora si suala la afya ya mwili tu, bali linahusiana moja kwa moja na mustakabali wa kiuchumi na kijamii wa taifa. Taifa lenye watu walio dhaifu kimwili kutokana na lishe mbovu halitaweza kushindana katika nyanja za uzazi, uzalishaji, ubunifu, wala maendeleo ya muda mrefu.
Swali la Leo:
Ikiwa lishe duni inazidi kudhoofisha kwa kimya afya yetu ya uzazi na nguvu ya kiuchumi, sasa tujiulize: Kwa hakika, tunawalisha nini watoto wetu wa kesho?