Watu tisa wa familia moja waliofariki dunia baada ya kuteketezwa katika eneo la Ugunja, Siaya watazikwa katika kaburi la pamoja Ijumaa.

Tisa hao; mwanaume, mkewe na watoto wao saba waliteketezwa walipokwa wakilala nyumbani kwao Aprili, 23.

Mili ya tisa hao itazikwa nyumbani kwao katika eneo la Upanda, Sigomere. Mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Christopher Okello Owino, mwenye umri wa miaka 56, tayari amekamatwa.

Mshukiwa ambaye alikuwa ameenda mafichoni alikamatwa jijini Nairobi Mtaani Kibra tarehe 24. Kulingana na polisi walipokea taarifa kumhusu mshukiwa huyo kwamba huenda alihusika na tukio hilo. Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Ugunja eneo ambapo tukio lililofanyika.

Aidha mkewe mshukiwa mkuu huyo alikamatwa baada ya mafuta taa yanayoaminika kutumika katika tukio hilo kupatikana nyumbani kwake. Pia simu za mshukiwa zinazuiliwa na zitatumika katika uchunguzi.

Inaarifiwa Owino aliwatafuta watu akawalipa kisha akasafiri nao hadi Ugunja ambapo walitekeleza kitendo hicho cha kinyama.