Familia ya marehemu Isaiah Kiplangat Cheluget imejitokeza hadharani na kuthibitisha kuwa inaunga mkono mpango wa Rais William Ruto, kuhusu kuuza ekari 5,800 za ardhi iliyoko Kaunti ya Narok kwa serikali ili kuwasaidia wananchi wasio na mashamba.

Wakati wa ziara yake katika kituo cha biashara cha Sogoo Alhamisi, Mei 8, Rais Ruto alizua gumzo mitandaoni baada ya kusema kuwa alifanya mashauriano na marehemu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Nyanza kuhusu ununuzi wa ardhi hiyo kwa ajili ya kuwahamisha na kuwapa ardhi wakazi waliopo.

“Mimi najua tuko na matatizo… tuko na shamba hapa ya Cheluget imetuletea matatizo siku mingi. Tumeita Cheluget, tumeketi chini na yeye, tumekubaliana hiyo shamba tutanunua kama serikali,” alisema Ruto huku akishangiliwa na wakazi.

Kauli hiyo ilizua maswali mengi miongoni mwa Wakenya waliokumbuka kuwa Cheluget alifariki dunia Juni 26, 2017, katika Hospitali ya Aga Khan mjini Kisumu.

Hata hivyo, familia ya marehemu imejitokeza Jumamosi, Mei 10, ikifafanua kuwa mazungumzo hayo yanaendelea kwa njia rasmi kupitia kwa wawakilishi wao waliokutana na maafisa wa serikali kwa nyakati tofauti tofauti.

Wakiongozwa na Balozi Nancy Kirui, familia hiyo ilithibitisha kuwa tayari wamekutana na Katibu wa Wizara ya Ardhi Nixon Korir, Gavana wa Narok Patrick Ntutu, na Mkurugenzi wa Masuala ya Uhamisho, Kennedy Njenga, kwa nia ya kupata suluhu ya kudumu kuhusu ardhi hiyo.

“Marehemu baba yetu aliwahi kuanzisha mazungumzo na serikali kutafuta suluhu ya amani. Bahati mbaya alifariki kabla ya kufikia muafaka. Sisi kama familia tumeendeleza juhudi zake,” alisema Kirui.

Familia pia imekana madai ya Moses Kipkirui, aliyedai kuwa ni mwana wa marehemu na kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi yake. Familia imesema Kipkirui hana nafasi yoyote katika usimamizi wa mali ya marehemu.

Walibainisha kuwa Mahakama ya Juu ya Kericho mwaka 2018 iliwateua rasmi Raeli Chepkurgat Cheluget (mjane wa marehemu), pamoja na Johnstone Kipkoech Langat, Laurence Kimutai Langat na Kenneth Kipyegon Langat kuwa wasimamizi halali wa mali ya marehemu Cheluget.

Kwa msingi huo, familia imesisitiza kuwa mazungumzo na serikali yanafanyika kwa mujibu wa sheria, huku wakiwashukuru Rais Ruto na Gavana Ntutu kwa juhudi zao za kutafuta suluhu ya haki na amani kwa mgogoro huo wa ardhi.