Elizabeth Ouma, mama wa Brian Odhiambo,ameachwa na majonzi baada ya Mahakama ya Nakuru kuwaachilia kwa dhamana maafisa sita wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), wanaodaiwa kumteka nyara mwanawe Januari 18, 2025.

Maafisa hao — Francis Wachira, Alexander Lorogoi, Isaac Ochieng, Michael Wabukala, Evans Kimaiyo na Abdulrahman Sudi — wameshtakiwa kwa kosa la kumteka mtu kwa nia ya kumficha kinyume cha sheria.

Katika kikao kilichofanyika Jumatatu, Mei 12, 2025, kilichojaa hisia kali, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na mawakili kutoka kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Chama cha Wanasheria (LSK), Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la IMLU, Vocal Africa na familia ya mwathiriwa, ulipinga kuachiliwa kwa washukiwa. Wakili wa familia, Kipkoech Ng’etich, alieleza kuwa familia hiyo ilishawishiwa kuhongwa ili kuondoa kesi hiyo, ishara ya vitisho na ushawishi wa kisiasa au wa kifedha.

Walionya kuwa kuachiliwa kwa maafisa hao kunaweza kuhujumu uchunguzi kwani eneo la tukio bado liko chini ya usimamizi wa KWS, ambako washukiwa wanaendelea kufanya kazi. Pia walieleza kuwa familia ya mwathiriwa na mashahidi ni raia wa kawaida wasiokuwa na kinga wala ushawishi kama walionao maafisa wa serikali.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Leon Kalisto wa KWS, ulieleza kuwa wateja wao wako tayari kushirikiana na uchunguzi na hawana nia ya kutoroka au kuingilia ushahidi.

Licha ya pingamizi hizo, Jaji Kibelion aliamua kuwa hakuna msingi wa kisheria wa kuwanyima dhamana, akisema haki za washtakiwa bado zinalindwa na katiba iwapo hakuna ushahidi wa kutosha wa kuwatenga.

“Kwa hivyo, kila mshtakiwa atakuwa huru kwa dhamana ya Sh300,000 na mdhamini wa kiasi sawa, au mbadala wa Sh100,000 pesa taslimu. Washtakiwa wamepigwa marufuku kuwasiliana na mashahidi wa upande wa mashtaka moja kwa moja au kwa njia nyingine. Pia hawataruhusiwa kuzuru eneo la tukio hadi kesi itakaposikizwa na kuamuliwa,” aliamuru Jaji Kibelion.

Written by, Allan Wetungu