Wakazi katika eneo la Githogoro, Nairobi wameandamana leo Jumanne na kufunga Barabara ya Nothern Bypass wakilalamikia kukosa huduma za umeme kwa takriban miezi sita sasa.
Wakiwa wenye hamaki, wakazi hao wameyateketeza magurudumu barabarani na kuifunga barabara ya kuelekea Ruaka kwa mawe hali iliyoathiri usafiri wa magari na watu huku wakiahidi kuendelea na maandamano hadi kilio cha kisikizwe.
Kulingana na wakazi hao, walikatiwa umeme na Kampuni ya Kusambaza umeme nchini, Kenya Power kwa madai kuwa kunao ambao hawalipi ada za umeme hali ambayo wanasema si haki kwani wengi wao wanalipia huduma hiyo.
”Ndio kunao ambao wamekataa kulipia umeme ila si vyema kukatia Kila mtu, kwani wengi wetu tunapa,” Brian Shitendi, Mkazi Githogoro.
Aidha wameishtumu hatua hiyo ya Kenya Power wakisema biashara zao zimethirika,huku wanafunzi wakikosa kusoma vizuri kwa kukosa mwanga.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wanasema kuwa wizi na uhalifu umeongezeka hata zaidi kwani wengi wao wameibiwa hasa nyakati za usiku. Wanasema kuwa wezi wanawahangaisha sana kutokana na kukosekana na umeme.
”Biashara zetu zimeathirika pakubwa na giza linapoingia wizi unazidi. Juzi kuna wale ambao wameibiwa simu zao. Usalama haupo kabisa. Tunaomba viongozi wetu watuangalia!” Damaris Nelima, mkazi.
Kulingana na wakazi hao, sehemu nyingine wanazopakana nazo mfano Runda zina umeme huku wakiitaja hali hii kuwa ubaguzi kutokana na hali yao duni ya kimaisha.
Wanatoa wito kwa viongozi wao na serikali ya kaunti kulishughulikia suala hilo na kuhakikisha kuwa wanarejeshewa nguvu za umeme la sivyo wataendelea kuandamana hadi kilio chao kitakaposikilizwa.
Written by, Silas Kemboi