Mahakama jijini Nairobi imetoa agizo la kupelekwa nchini Marekani kwa raia mmoja wa Afghanstan nchini Marekani anakokabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya na umiliki wa silaha kinyume cha sheria.
Katika uamuzi wake, Hakimu Mkuu Benmark Ekhubi, Jumanne alikubaliana na uamuzi uliokuwa umetolewa nchini Marekani wa kutaka Abdul Zahir Qadeer, anayejuikana kwa jina jingine Haji Abdul Zahir kuwasilishwa nchini humo.
Ofisi ya DPP kupitia wakili wake Victor Owiti, aliwasilisha ushahidi mahakamani ambapo aliishawishi kwamba makosa yanayomkabili mshukiwa yanatosha kwake kupelekwa Marekani kufunguliwa mashtaka.
Owiti aliiomba mahakama kukubali kumpeleka marekani mshukiwa huyo ili afunguliwe mashtaka. Aidha aliiambia mahakama kwamba Abdul Zahir Qadeer anaweza kupata nafasi ya kujitetea iwapo atashtakiwa Marekani.
Mahakama ya jimbo la New York ilikuwa imetoa agizo la kukamatwa kwa mshukiwa huyo.
Kitengo cha Polisi wa Kimataifa cha Interpol pia kilita agizo la kimataifa la kukamatwa kwake Aprli 14, 2025. Maagizo hayo yalitekelezwa wakati mshukiwa alipokamatwa jijini Nairobi katika Hoteli ya Safari Park.