Mwanafunzi wa kidato cha tatu ameuliwa na nduguye wa gredi ya sita kujeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa nyumbani kwao katika eneo la Olando, Kaunti ya Homa Bay.
Mwanafunzi huyo ambaye ametambuliwa kuwa Alphins Opuodho, mwanafunzi wa Shule ya Upili ya St Joseph’s Olando anasemekana kuuliwa kwa kudungwa kisu na mwanaume anayeaminika kuwa mpenzi wake, Jumanne saa tano unusu.
Inaaminika kuwa mwanaume huyo alitofautiana na msichana huyo kabla ya kumuua.
Naibu Chifu wa Lokesheni ya Kibwer Richard Okinyi amesema, mshukiwa alivamia nyumba ambako msichana huyo alikuwa akilala na nduguye kisha kumuua kwa kumdunga kisu kichwani na mgongoni.
Baada ya hapo msichana huyo mshukiwa alimvamia nduguye mdogo kisha kumdunga na kumjeruhi vibaya kwenye mkono na tumbo kabla ya kutoweka.
Wakazi waliwakimbiza wawili hao katika hospitali ya Magunga Level Four ambapo msichana huyo alithibitishwa kufariki dunia.
Hata hivyo, mshukiwa hajajulikana kwa kuwa familia ya msichana aliyemuua haikuwa inamfahamu.
Naibu Chifu huyo amesema wamewarifu polisi kuhusu tukio hilo na uchunguzi umeanzishwa. Mwili wa msichana aliyeuliwa umepelekwa katika Hifadhi ya maiti ya Hospitali ya St Camillus.