Vita dhidi ya biashara haramu ya mihadarati na unywaji pombe nchini vimepamba moto kufuatia msako mkali katika Kaunti za Kisii na Homa Bay.
Katika msako wa kwanza uliopangwa na kuongozwa kutokana na taarifa za kijasusi huko Oyugis, Kaunti ya Homa Bay, maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabili Matumizi ya Dawa za Kulevya na Unywaji Pombe NACADA kwa ushirikiano na Kitengo cha Kukabili Dawa za Kulevya ANU na Idara ya Polisi wa Utawala APS waliwakamata watu wawili waliokuwa na dawa zinazoshukiwa kuwa za kulevya pamoja na bidhaa za magendo.
Aidha maafisa walikamata pakiti 400 za sigara zisizo na stempu ya ulipiaji kodi, pakiti 14 za sigara maarufu, pamoja na kiasi cha pesa katika noti mbalimbali kinachoshukiwa kuwa mapato ya biashara haramu. Mmoja wa washukiwa pia alipatikana na bangi.
“The contraband cigarettes are believed to have been smuggled into the country without customs clearance, in violation of revenue and trade regulations,” NACADA ilisema.
Washukiwa hao wawili kwa sasa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oyugis huku uchunguzi ukiendelea.
Wakati uo huo, katika Kaunti ya Kisii, oparesheni tofauti iliyoongozwa na NACADA kwa ushirikiano na Idara ya Polisi NPS, Idara ya Upelelezi DCI na ANU ilibaini mahali panapoaminika kutumika kuhifadhi dawa za kulevya.
Katika msako huo uliofanyika katika nyumba ya kukodi kijijini Nyakongo, eneo la Kitutu Central, Misokoto 134 mikubwamikubwa ya bangi ilipatikana pamoja na magunia mawili ya kilo 90 ya bangi iliyokaushwa.
Washukiwa wanane walikamatwa wakati wa oparesheni hiyo ya Kisii na kwa sasa wanazuiliwa na polisi wakisubiri kuwafikishwa mahakamani.
Oparesheni hizi zinafanyika mwezi mmoja tu baada ya kuvunjwa kwa mtandao mkubwa wa usambazaji wa dawa za kulevya katika Kaunti ya Kisii uliokuwa ukihusishwa na mfanyabiashara maarufu wa bidhaa hiyo haramu.
NACADA imesema kukamatwa kwa washukiwa hao ni uthibitisho wa “mwendo wa kimkakati” wa mamlaka hiyo kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kulinda jamii dhidi ya athari za uraibu wa dawa.
“NACADA continues to champion a multi-agency approach to narcotics control, collaborating closely with law enforcement and intelligence partners to protect communities from the harmful grip of drugs,”
Mamlaka hiyo inawahimiza wananchi kuwa waangalifu na kuripoti shughuli zozote zinazohusiana na dawa za kulevya kwa siri kupitia nambari ya bure ya simu 1192.