Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amechagua chama kipya cha kisiasa kiitwacho Democracy for Citizens Party (DCP) kuwa chombo chake rasmi cha kisiasa.

Gachagua, aliyejiuzulu kutoka chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) Mei 12, 2025, anatarajiwa kukizindua chama hicho kipya katika makao makuu ya DCP yaliyoko Barabara ya Musa Gitau, Lavington, Alhamisi, Mei 15 kuanzia saa tatu asubuhi.

Gachagua pamoja na wandani wame wamefichukua kuwa wamekubalina ana jina DCP, chama kilichosajiliwa rasmi Februari 3, 2025.

Rangi rasmi za chama hicho ni kijani, kahawia na nyeusi, huku nembo yake ikiwa ni mkono unaogusa sikio, kuashiria “kusikiliza wananchi.” Kauli mbiu ya chama hicho ni Kazi na Haki. Gachagua ambaye alitimuliwa ameendeleza ujumbe wa kisiasa unaozingatia kusikiliza wananchi.

Ingawa mahali pa hafla ya uzinduzi bado hakujatangazwa rasmi, taarifa zinaashiria kuwa Gachagua huenda akatangaza jina la chama hicho Alhamisi, Mei 15, 2025, huku akipanga tamasha kubwa la uzinduzi rasmi baadaye mwezi huu.

Kabla ya hafla hiyo, Gachagua na wandani wake walikuwa katika kikao cha faragha Jumanne jioni kupanga muundo wa uongozi wa chama hicho na kujaza nafasi muhimu.

Wale waliotajwa kuwa wanachama wa bodi ya uongozi ya DCP ni: Thomas Ratemo, Ado Yiembo, Mably Owino, Hussein Athman, Laura Njeri, Abdifatah Abdullahi, Joy Gatugi, Jeremiah Mong’eri, Joel Sang, John Maranga, Miriam Fredina Mariki, na Brenda Banjira Omusinda.

Gachagua ananuia kukitangaza chama hicho kwa upana ili kushirikiana kisiasa na viongozi wa upinzani akiwamo Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP), Eugene Wamalwa (DAP-Kenya), na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang’i anayepigiwa upatu kuwania urais mwaka 2027.