Wakazi wa Kaunti ya Mombasa Jumatano, walikuwa miongoni mwa Wakenya katika kaunti mbalimbali ambao walishiriki shughuli ya kutoa maoni kuhusu ongezeko la ukatili, dhulma za kijinsia na mauaji ya kiholela dhidi ya wanawake.

Wakazi, makundi ya kiraia, ya kidini na hata waathiriwa walitoa maoni mbalimbali, likiwamo pendekezo la maafisa wa polisi kupewa mafunzo maalum jinsi ya kushugulikia visa hivyo, huku wito ukitolewa kwa idara ya mahakama kuharakisha kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hizo angalau ndani ya kipindi cha miezi sita.

Shughuli ya kutoa maoni iliendeshwa katika ukumbi wa Tononoka, ikisimamiwa na wawakilishi wa jopo maalum, lililoteuliwa na Rais William Ruto kuangazia na kutatua ongezeko la dhulma za kijinsia, hasa mauaji ya wanawake, ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Wanawake zaidi ya 600 waliripotiwa kuuliwa na wanaume kati ya mwaka wa 2016 na 2024, mwaka wa 2024 ukitajwa kuwa uliokuwa na visa vingi vya mauaji ya kiholela ya wanawake, visa zaidi ya 160 vikiripotiwa.

Jumla ya mashirika 9 yanayotetea haki za wanawake katika Kaunti ya Mombasa yaliwasilisha nakala za mapendekezo kwa jopo hilo, mengi yakiangazia kutathminiwa upya na kuimarishwa kwa mfumo wa kuwaadhibu wanaopatikana na hatia ya mauaji hayo, kuharakishwa kusikilizwa na kutatuliwa kwa kesi hizo, pamoja na kutolewa mafunzo kwa maafisa wa polisi jinsi ya kushugulikia visa hivyo.

Topista Juma, anawakilisha jopo kazi la Kaunti ya Mombasa la kushugulikia dhulma za kijinsia.

“Tunaomba kutathminiwa upya kwa kanuni ya adhabu ili ijumuishe dhulma dhidi ya wanawake kama kosa la mauaji, na washukiwa kushtakiwa na kosa hilo. Tunaomba pia waathiriwa wa visa hivi kupokea huduma bila malipo, hasa za matibabu. Isitoshe, tunaomba kuwapo kwa mahakama maalum ya kushugulikia kesi za ukatili wa kijinsia, dhulma na mauaji ya wanawake katika kila kaunti, ili kesi hizo ziweze kusikilizwa na kutatuliwa kwa haraka.” 

Elizabeth Atieno, wa vuguvugu la kupinga mauaji ya wanawake naye amependekeza serikali kubainisha dhulma za kijinsia, kwani nyingi za dhulma hizo hazitambuliwi katika mfumo wa adhabu za kisheria, hali ambayo ni kikwazo kikubwa katika ufuatiliaji wa visa hivyo na kusababisha waathiriwa wengi kukosa haki. Aidha, Amependekeza kuondolewa kwa sheria nyingi za ushahidi wa waathiriwa wa visa kama vile ubakaji na dhulma zingine, kwani wengi hawajui masharti ya kuripoti visa hivyo.

“Ufafanuzi wa ukatili wa kijinsia (GBV) nchini hauhusishi dhulma dhidi ya wanawake ambazo huishia kusababisha vifo na visa vingine vya mauaji, jambo ambalo linawafanya waathiriwa kupata ugumu wa kuripoti. Tunaomba pia serikali iondoe sheria nyingi za ushahidi, kwa visa kama vile ukatili wa kingono, kwani watu wengi hawajui kuwa kisheria mtu hapaswi kuoga baada ya kisa ili kuhifadhi ushahidi. Ni lazima wakenya wahamasishwe ili kuondoa unyanyapaa”

Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa Zamzam Mohammed, alihudhuria shughuli hiyo, ambapo alitoa wito kwa jamii kuasi tamaduni zilizopitwa na wakati, zinazomkandamiza mwanamke, huku akiwataka wanaume kuwaheshimu wanawake na kutafuta mbinu mbadala za kusuluhisha tofauti panapo na mgogoro.

Shughuli ya kukusanya kura ya maoni kuhusu ongezeko la ukatili, dhulma za kijinsia na mauaji ya kiholela dhidi ya wanawake katika kaunti mbali mbali inatarajiwa kukamilika wiki ijayo, ambapo mchakato wa kuunda ripoti utafuata, ikijumuisha mapendekezo ya sera na sheria za kukabiliana na visa hivyo.

Written by, Paul Muniu