Maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC wamewakamata maafisa wakuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi kufuatia uteuzi uliokiuka sheria wa Daniel Brian Ouma Okeyo kuwa Kaimu Mkuu wa Mipango.

Miongoni mwa wale waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Profesa Amukowa Anangwe, Daniel Brian Ouma, na wanachama wengine wawili wa baraza hilo ambao ni Ahmed Sheikh Abdullahi na Carren Kerubo Omwenga.

Wanne hao huenda wakakabiliwa mashtaka ya kukiuka agizo la mahakama lililotolewa Aprili 8, mwaka huu wa 2025.

Profesa Anangwe alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu na wengine wakitiwa mbaroni jijini Nairobi.

Kulingana na EACC wanne hao walipuuza mamlaka ya Baraza la chuo na barua iliyotumwa na Naibu Mkuu Stephen Kiama kisha kumwajiri Ouma.

Ouma anakabiliwa na tuhuma za kugushi stakabadhi za masomo na kunyakua mali ya umma yenye kima ya thamani ya shilingi milioni 32 (ikiwa ni mshahara aliolipwa kati ya mwaka 2015 na 2025).

Inaarifiwa alilipwa fedha hizo akiwa anashikilia nyadhfa mbalimbali chuoni humo ilhali hakuwa amehitimu.

Washukiwa watafikishwa mahakamani Ijumaa alasiri. Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi limekuwa likishtumiwa kwa kukiuka ushauri wa EACC dhidi ya kumwajiri Ouma baada ya maswali kuibuliwa kuhusu viwango vyake vya elimu.

Â