Serikali kupitia Wizara ya Utalii na Wanyamapori inaendeleza juhudi za kuwafidia waathiriwa wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori kwenye Kaunti ya Taita Taveta. Waziri Rebecca Miano akiongoza shughuli ya kutoa hundi ya pesa za fidia kwa waathiriwa wa kaunti hiyo ya takribani shilingi milioni arobaini na tano kwa familia ishirini na mbili.

Akihutubia umati uliofika katika hafla hiyo mjini Mwatate Alhamisi tarehe 15, Miano alisema serikali ya Rais William Ruto imeweka mikakati ya kutimiza ahadi ya kulipa fidia kwa walioathiriwa na wanyamapori.

“Tumeweza kupiga hatua kwenye mchakato wa ulipaji fidia, na kwa wale ambao bado hawajalipwa, serikali inashughulikia mchakato huo kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” alisema waziri Miano.

Kauli yake ilisisitizwa na Katibu Mkuu wa Utalii na Wanyamapori Sylvia Museiya akisema kuwa serikali ya sasa imefanya kipaumbele mpango wa kutoa fidia kwa wakati, tofauti na serikali ya awali ambayo alidai haikutilia maanani suala hilo.

“Utawala huu umeonyesha kujitolea, si kwa kutoa fedha pekee, bali pia kuhakikisha mchakato unakuwa wa haraka na wa haki,” alisema Bi Museiya.

Baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika nje ya ofisi ya Kamishina wa Kaunti Josphine Onunga, wakiongozwa na Naibu Gavana Christine Kilalo ni Mbunge wa Mwatate Peter Shake, Mbunge wa Voi Khamisi Chome, Mwakilishi Wadi ya Chawia Joseph Mabishi, Mwakilishi wa Wadi ya Mwatate Joseph Mwalegha Ankoo, Mwakilishi Maalum Peter Shambi na Patricia Mwashighadi na Mwakilishi wa Ofisi ya Lydia Haika Doreen Righa.

Viongozi hao wa kaunti aidha waliitaka wizara kupunguza muda unaochukuliwa kufidia familia zilizoathirika, vilevile kupendekeza mnyama aina ya njoka kurudishwa katika orodha ya Wanyama hatari wanaostahili kufidiwa.

Suala la Ua la Umeme lilizungumziwa, mradi huo ukisemekana kwamba unaendelea hivi sasa na  serikali imeweka bajeti ya kutosha kuhakikisha mradi huo unakamilishwa kuanzia sehemu ya Alia hadi Kasigau.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS), Dkt. Erastus Kanga alihakikishia umma kuwa shirika hilo linaendelea kulinda maisha ya watu na wanyamapori kwa pamoja.

Alisema Kaunti ya Taita Taveta inashika nafasi ya pili kwa kuathirika zaidi na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori baada ya Kajiado, na mbele ya Narok, Laikipia, Meru, Isiolo na Makueni.

“Tunaendelea pia kuchimba mabwawa ya maji ndani ya hifadhi ili kuhakikisha wanyama wanapata maji huko na wasielekee kwenye makazi ya watu,” alisema Dkt. Kanga, huku akimpongeza Rais Ruto kwa kuunga mkono uhifadhi wa wanyamapori na mpango wa fidia.

Naibu Gavana wa Taita Taveta, Christine Kilalo alitoa wito kwa serikali kuu kuanzisha mfuko wa dharura kusaidia wakazi wanaojeruhiwa na wanyama pori wakati wakisubiri fidia. Alipendekeza pia kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Fidia ya Wanyamapori ili kujumuisha wanyama wadogo lakini waharibifu kama nyoka, tumbili na nyani.

Kilalo pia alitaka kuwe na mgao wa mapato wa asilimia 50/50 baina ya serikali za kaunti na ya kitaifa kutoka kwa mapato ya utalii wa wanyamapori, na pia kutaka wakazi wa maeneo jirani na mbuga wapewe kipaumbele kwenye nafasi za kazi katika miradi ya uhifadhi.

Written by, Julius Mariki