Wakazi wa kijiji cha Oduo, Eneo Bunge la Muhoroni, wanalalamika kufuatia ukosefu wa kituo cha afya na hali mbaya ya barabara . Wakazi hao wanatoa wito kwa viongozi wa Kaunti ya Kisumu na Serikali ya Kitaifa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wanapata huduma bora za matibabu namuundo msingi.
Kituo cha Afya cha Oduo, ambacho kilijengwa mwaka wa 2015 chini ya uongozi wa gavana wa kwanza wa Kisumu, Jack Ranguma, kilikuwa tegemeo kwa maelfu ya wakazi wa eneo hilo. Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, kituo hicho kimetelekezwa na sasa ni makao ya bwanyama pori, huku wakazi wakilazimika kusafiri kilomita nyingi kutafuta matibabu katika vituo vya mbali.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, hali hiyo imewalemea sana, ikizingatiwa kuwa barabara inayoelekea kwenye maeneo ya huduma za afya haipitiki, hususan wakati wa mvua. Wanadai kuwa ukosefu wa muundo-msingi bora umesababisha vifo vya watu waliokuwa wakijaribu kufika hospitali kwa matibabu ya dharura.
“Tunateseka sana. Watu wanakufa njiani wakielekea Muhoroni au Kisumu kutafuta huduma za afya. Hatuwezi kuendelea kuishi kwa namna hii,” alisema mkazi mmoja kwa masikitiko makubwa.
Wakazi sasa wanatoa wito kwa viongozi wa ngazi zote, kuanzia uongozi wa kaunti hadi Serikali ya Kitaifa, kuingilia kati na kuhakikisha kuwa kituo cha afya cha Oduo kinafanyiwa ukarabati na kupatiwa wahudumu wa afya pamoja na dawa za kutosha. Aidha, wanasisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa barabara ili kurahisisha usafiri na upatikanaji wa huduma za msingi.
“Tunahitaji serikali itusikie. Tunahitaji wahudumu wa afya, dawa, na barabara bora,” akaongeza mkazi mwingine.
Hali hii inaibua maswali kuhusu uwajibikaji wa serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya na miundombinu bora, huku wakazi wa Oduo wakisalia na matumaini kuwa sauti zao zitasikika na mabadiliko yatafanyika.
Written by, Laban Shikokoti